Bao la kideoni lamvuruga Jaap Stam

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo kati ya mechi 10 walizocheza amefunga mabao manne sawa na nyota wa Simba,Meddie Kagere na kuingia katika orodha ya wafungaji Bora hadi sasa akitanguliwa na Eiud Ambokile wa Mbeya City mwenye mabao sita.

KOCHA wa Mbao, Amri Said ‘Jaap Stam’ ameangalia kwa makini bao lililofungwa na nyota wake, Said Khamis juzi wakati wakiichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 katika Uwanja wa CCM Kirumba na kusema ni la kiufundi na kwa upande wake anaona ni bora hadi sasa.

Straika huyo alifunga bao hilo lililoipa timu yake ushindi, huku wadau wakilinganisha na lile la nyota wa Yanga Ibrahimu Ajibu alilofunga dhidi ya Mbao, lakini Kocha Said alisema la nyota wake ndilo matata zaidi hadi sasa.

Kocha huyo alisema hadi sasa anaona hilo ndilo bao pekee bora kutokana na mchezaji alivyoupokea mpira na kutulia kisha kufunga kiufundi kama alivyofanya.

“Niwapongeze wachezaji wangu kwa jinsi walivyopambana kupata matokeo mazuri katika mechi ngumu ya leo (juzi), lakini niseme kwamba bao hili ni bora kati ya mabao yaliyofungwa hadi sasa katika Ligi Kuu,” alisema Said.

Naye mfungaji wa bao hilo ambaye ni msimu wake wa pili akiwa na Mbao, alisema hakubahatisha kufunga bao hilo, isipokuwa kwa jinsi alivyopokea mpira ilimlazimu kufanya hivyo.

Aliongeza yeye kama straika kazi yake ni kufunga bila kujali staili na malengo yake ni kuisaidia timu kupata matokeo mazuri, lakini pia kuwania tuzo ya kiatu cha Mfungaji Bora mwishoni mwa Ligi.

“Naangalia mafanikio ya timu na kujitahidi kuisaidia, kuhusu bao hili sijabahatisha Straika anafunga kwa staili yoyote.”