Bao la Yanga lampa dili Massawe

Muktasari:

Yanga ilikuwa haijapoteza mchezo wowote katika Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa imecheza mechi 19 na kushinda 17 na kupata sare mbili, lakini bao la Massawe la dakika ya 89 liliwamaliza.

KUZIFUNGA Simba na Yanga kuna raha yake bwana asikuambie mtu. Sikia kilichompata nahodha wa Stand United, Jacob Massawe baada ya kuwalaza mapema vijana wa Jangwani wikiendi iliyopita alipofunga bao pekee Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Massawe amefichua baada ya mechi hiyo ambayo Yanga ililala bao 1-0 na kutibuliwa rekodi yake ya kucheza mechi mfululizo bila kupoteza, alikutana na ‘supraizi’ ambayo hakuitegemea maishani mwake kwa kutafutwa na matajiri wa Mkoa wa Shinyanga na kukusanya pesa kutoka kwa mashabiki waliompa mkononi na wengine wakituma kwa njia ya simu.

Aliendelea kufichua siri nje ya kushikwa mkono na matajiri wa mkoa huo pamoja na mashabiki jana Jumatatu alienda kukutana na mdhamini wao Kampuni ya Jambo, aliyedai kumpigia simu aende ofisini kumpa mkono wa hongera kwa kazi nzuri ya kuifunga Yanga.

“Yanga imebadilisha maisha yangu kwa mara ya kwanza niliona kama niko ndotoni niliyokuwa natamani niwe mwanasoka ninayejulikana, nilishangaa watu wamepata wapi namba yangu mpaka wananipigia simu kiasi kile hadi nilikuwa najiuliza hivi hawa watu hawalali,” alisema Massawe aliyedokeza kwa hesabu za haraka si chini ya Sh 700,000 zmepewa kupitia ahsante aliyopewa kwa kuitungua Yanga.

Yanga ilikuwa haijapoteza mchezo wowote katika Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa imecheza mechi 19 na kushinda 17 na kupata sare mbili, lakini bao la Massawe la dakika ya 89 liliwamaliza.

“Nikipita mtaani naonekana wa tofauti, nimeamini Simba na Yanga zina nguvu kisoka, akili yangu imeamka na kuanza kutazama mbele zaidi nikiamini nitakuja kula matunda zaidi ya haya nilionayo, aisee hadi watu walikuwa wanatamani kupiga picha na mimi kitu ambacho sio kawaida sana kutokea kwangu,” alisema.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Athuman Bilal ‘Bilo’ naye hakutaka kuwa nyuma kama kawaida yake kutamba akidai jeshi lake ni hatari ndio maana limetibua rekodi ya kocha Mwinyi Zahera.

“Wakati Zahera amechukua tuzo ya Kocha Bora wa mwezi mara tatu mfulilizo nilisema nimejifunza kitu kwake na nitakuwa natumia mbinu zake, hivyo tukaamua kuanza na yeye mwenyewe kumuonjesha machungu ya kumfunga ili ajue ligi ina kicheko na huzuni,” alisema.