Bandari yaonya Wasudani mapema

Muktasari:

Wakati huohuo, Mwatate United FC imekamilisha mechi zake za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza ikiwa na matumaini makubwa ya kupanda hadi Supaligi ya Taifa msimu ujao unaotarajia kuanza Septemba.

Mombasa. BINGWA wa SportPesa Shield, Bandari FC inajitayarisha kwa mechi yake ya Caf Confederation Cup dhidi ya timu ya Al-Hilal ya Sudan itakayochezwa kati ya Agosti 8-10.

Kulingana na Naibu Kocha wa Bandari FC, Nassoro Mwakoba baada ya wiki moja ya mapumziko, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi walirudi na kuanza mazoezi jana Jumatatu kujiandaa kwa mchuano huo wa kupigania taji la barani Afrika.

“Baada ya likizo ya wiki moja, timu imerudi uwanjani na kuanza kujitayarisha kwa mechi ya dimba la barani Afrika. Tunataka tupate ushindi dhidi ya timu hiyo ya Sudan tusonge kwenye raundi nyingine,” alisema Mwakoba.

Lakini mkufunzi huyo hakuweza kuthibitisha kama watacheza mechi mbili, ya nyumbani na ya ugenini ama itakuwa ni mechi moja ya ugenini pekee.

“Hilo siwezi kusema kwa sababu hatujafahamishwa kama tutacheza mechi mbili ama moja pekee uwanja wa ugenini kwa timu zetu mbili,” alisema Mwakoba.

Alipoulizwa kama kuna sajili mpya nyingine, kocha huyo alisema atafahamu watakapokuwa mazoezini.

“Kwa sasa sijui lolote juu ya sajili mpya mpaka pale tutakapokuwa mazoezini ndipo nitafahamu,” alisema Mwakoba.

Wakati huohuo, Mwatate United FC imekamilisha mechi zake za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza ikiwa na matumaini makubwa ya kupanda hadi Supaligi ya Taifa msimu ujao unaotarajia kuanza Septemba.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, James Okoyo alisema watapeleka ombi kwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kupitia kwa tawi lake la Pwani kuomba nafasi ya kushiriki kwenye Supaligi ya Taifa kama kutakuwako na nafasi itakayoachwa wazi.