Bandari FC yaweka makataa ya kuibanjua nje Sofapaka FC

Muktasari:

Kuhusu mchezo wao na Sharks, Muhiddin alisema alitabiri timu yoyote itakayoshinda utakuwa wa bao 1-0 na hivyo ndivyo ilivyotokea. “Imekuwa mechi ngumu huku wapinzani wetu wakitawala kipindi cha kwanza.

MOMBASA. BANDARI FC imepania kuhakikisha inahifadhi taji lake la kombe la FKF Cup kwa kufanya maandalizi kabambe ili iweze kuibanjua nje Sofapaka FC kwenye mechi itakayofanyika mwishoni mwa wiki hii.

Kocha Twahir Muhiddin alisema baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao wakubwa wa Kariobangi Sharks FC katika mchezo wa Ligi Kuu Jumamosi iliyopita, sasa wanaangazia mchezo wao na Sofapaka wakidhamiria kushinda kuendeleza harakati za kuhakikisha wanashinda tena kombe hilo.

“Tumefurahi kwa kuwashinda Sharks kwa bao 1-0 ambapo tumejisogeza juu kwa pointi hizo tatu na hivi tumeshaanza mikakati ya kuhakikisha tunapata ushindi tutakapopambana na Sofapaka kwenye mchezo wa FKF Cup uliojulikana kama SportsPesa Shield,” akasema.

Kuhusu mchezo wao na Sharks, Muhiddin alisema alitabiri timu yoyote itakayoshinda utakuwa wa bao 1-0 na hivyo ndivyo ilivyotokea. “Imekuwa mechi ngumu huku wapinzani wetu wakitawala kipindi cha kwanza.

“Lakini baada ya kuongea na wachezaji wetu wakati wa mapumziko, nashukuru walisikiliza mawaidha tulowapa na wakaweza kuwazuia wapinzani wao na mwishowe kupata ushindi huo mwembamba,” alisema Muhiddin.

Kocha wa Kariobangi Sharks, William Muluya alisema walicheza vizuri zaidi ya wapinzani wao lakini washambuliaji wao hawakutumia nafasi walizopata za kufunga mabao.

 “Hivi sasa tunakwenda kurekebisha makosa yaliyofanyika ili tuweze kushinda mechi zetu zilizobakia,” alisema Muluya.

Bao la pekee la ushindi kwa upande wa Bandari ilifungwa na straika wao mpya John Mwita, ambaye wiki ya nyuma alikuwa ameifungia timu hiyo ya Pwani mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KCB katika Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.

Mshindi wa kombe hilo anaiwakilisha Kenya kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika na Bandari inaamini hiyo ndio tiketi ya kushiriki.