Bandari FC yaanza kuweka maandalizi kabambe ya ligi

Monday November 5 2018

 

BAADA ya kumaliza mapumziko, kiungo wa Bandari FC, Abdallah Hamis amerejea jana Jumapili nchini Kenya kujiunga na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Kenya wa 2018/19.

Hamis aliwahi kuichezea Sony Sugar ya nchini humo, alisema wenzake walianza maandalizi ya msimu huu, Jumatatu ya wiki iliyopita na anatarajia kuungana nao leo Jumatatu.

“Kambi ya awali ilianza kwa wachezaji wa ndani, wale ambao tunatoka nje ya Kenya walitusogezea muda na kuhusu programu za mazoezi lazima zitakuwa za kurejesha utimamu kwanza ( physical) ,” alisema kiungo huyo.

Hamis aliwahi kuitwa na kuichezea Taifa Stars, iliyokuwa chini ya Salum Mayanga, amepanga huu uwe msimu wake wa mwisho Kenya kabla ya kwenda kukabiliana na changamoto nyingine za soka kwingine.

Kiungo huyo, alisema atafurahi kama ataondoka Kenya akiwa ametwaa taji la Ligi Kuu ambalo msimu uliopita walitwaa Gor Mahia inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr.

Advertisement