Bandari FC kambi ni Afrika Kusini

Muktasari:

  • Tetesi zilizokuwako hapo awali ni kuwa ni baadhi ya wachezaji ndio watakwenda Afrika Kusini lakini Ofisa Mkuu Mtendaji wa Bandari FC, Edward Oduor alisema hiyo ilikuwa ziara ya kujitayarisha kwa msimu mpya na hivyo wachezaji wote watakwenda.

MOMBASA. KIKOSI kizima cha wanasoka 30 cha Bandari FC kinatarajia kusafiri hadi Afrika Kusini ambako kinatarajia kupiga kambi ya mazoezi na kucheza mechi kadhaa za kirafiki ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya maandalizi ya msimu ujao wa 2019-2020.

Tetesi zilizokuwako hapo awali ni kuwa ni baadhi ya wachezaji ndio watakwenda Afrika Kusini lakini Ofisa Mkuu Mtendaji wa Bandari FC, Edward Oduor alisema hiyo ilikuwa ziara ya kujitayarisha kwa msimu mpya na hivyo wachezaji wote watakwenda.

“Hiki ni kipindi cha kumpa fursa kocha wetu Bernard Mwalala kuwa na nafasi ya kujionea hali ya kila mchezaji ilia pate kuchaguwa kikosi cha wanasoka wake watakaowakilisha timu yetu kwa msimu ujao,” akasema Oduor.

Kati ya wachezaji wanaotarajia kuwako kwenye msafara huo ni sajili zao mbili mpya, kiungo Danson Chetambe kutoka Zoo Kericho na winga Wycliffe Kasuti kutoka Sofapaka ambao wamekamilisha usajili wao na Bandari.

Oduor hakuweza kuthibitisha ni lini timu hiyo itaondoka nchini lakini alisema itakuwa wakati wowote wiki ijayo.

“Tuko kwenye mipango ya safari ya kwenda huko Afrika Kusini na tunaazimia kuondoka wiki ijayo,” akasema.

Kuhusu mjadala unaoendelea wa golikipa Farouk Shikalo, kwa mara nyingine Oduor ametoa onyo lingine kwa klabu ya Young Africans (Yanga) kukoma kutangaza kipa huyo kuwa ni wao ama wameshamsajili na huenda wakachukua hatua za kisheria.

“Ninavyofahamu Shikalo yuko kwa timu ya taifa ya Harambee Stars huko Misri na yungali ni mchezaji wetu halali na kamwe hatutanyamaza kimya ikiwa Yanga itamsajili kupitia mlango wa nyuma.

“Kuna mkataba kati ya Shikhalo na Bandari FC na mkataba huo lazima uheshimiwe. Timu yoyote inayotaka kumsajili ni sharti ifuate kanuni zinazohitajika. Atakayekwenda kinyume na mkataba huo, tutamchukua hatua za kisheria,” akasema.