Bandari, Gor Mahia zanasa vifaa usajili mpya

Thursday April 11 2019

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

MOMBASA. MATANO Abdalla jana alithibitisha amesajiliwa na timu ya Ligi Kuu ya SportPesa ya Bandari FC kutoka klabu ya Congo Boys ambayo inashiriki kwenye Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza.

Abdalla aliliambia Mwanaspoti anafurahikia kusajiliwa na Bandari kwa sababu anaamini ataweza kuinua kipaji cha uchezaji wake kwa haraka mbali na kuonekana na maskauti wanaohudhuria mechi za Ligi Kuu ya SportPesa.

“Nimeshatia saini hati za kuichezea Bandari na nimeanza mazoezi na timu yangu hiyo mpya na nina imani kubwa kama nitaendeleza kipaji cha uchezaji wangu. Nitafanya bidi kuhakikisha naichezea timu yangu mpya kwa moyo wangu wote,” akasema mwanasoka huyo.

Akiwa golikipa, Abdalla alisema anafurahikia kuona anajiunga na timu ambayo ina golikipa mzuri Farouk Shikhalo anayechezea timu ya taifa ya Harambee Stars na kocha mzoefu wa makipa Razak Siwa aliyekuwa na mkufunzi wa Stars na klabu kadhaa marufu za Afrika Mashariki.

“Kuwako timu moja na Shikhalo na Siwa kutanisaidia pakubwa kuinua kipaji cha uchezaji wangu. Naamini nitaendelea kujifunza mengi kwa hao wawili ili tuisaidie Bandari yetu kufanya vizuri kwenye mechi zilizobakia za ligi kuu,” akasema Abdalla.

Abdalla aliyekuwako uwanja wa mazoezi wa timu aliyotoka ya Congo Boys FC aliwahi kuzichezea za Bandari Youth miaka ya 2015 na 2016, Nivas ya Nairobi msimu wa 2017 na Congo Boys msimu uliopita wa 2018.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally jana alipongeza hatua ya Bandari kumsajili Abdalla akiwa na matumaini klabu hiyo kuendelea kusajili chipukizi wa Mkoa wa Pwani.

Advertisement