Banda mguu mmoja nje Baroka

Monday February 11 2019

 

By Eliya Solomon

IMEFICHUKABaroka imeanza kujiandaa na maisha bila ya beki wake wa kutumainiwa Abdi Banda ambaye kwa mujibu wa taarifa za ndani, yuko mbioni kutimka.

Chanzo chetu kimebaini Banda amekuwa kwenye mvutano wa muda mrefu na viongozi wa Baroka ambao walimuomba aendelee kusalia kwenye klabu hiyo huku taratibu za kumtafuta mbadala wake zikiendelea.

Inadaiwa kusajiliwa kwa Vusi Sibiya, Oktoba mwaka jana kutoka Tshwane University of Technology, ulikuwa ni mpango wa kumuandaa ili azibe pengo la Banda mara baada ya kuondoka.

Hata hivyo, Sibiya amekuwa akifanya makosa mengi binafsi ambayo yanahatarisha usalama wa safu yao ya ulinzi ya kati ambayo imekuwa ikichezwa na Banda pamoja na Bonginkosi Makume.

“Kuna timu ambazo tayari zimeshatuma ofa za kumchukua Banda, ni vigumu kushindana nazo kwa sababu ni timu kubwa ambazo zinaweza kutengeneza ushawishi kw mchezaji moja kwa moja.

“Ataondoka muda wowote ndio maana tuliamua kumchukua Sibiya ambaye ni kijana ili aanze kuingia taratibu kwenye mfumo wa mwalimu,” alisema mtu huyo ambaye jina lake lilifichwa.

Miongoni mwa vigogo wa soka la Afrika Kusini ambao wamekuwa wakihitaji huduma ya Banda ni Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates, Kaizer Chiefs na SuperSport United.

Advertisement