Banda kiroho safi kutemwa stars

Muktasari:

  • Hata hivyo, Banda mwenyewe ameliambia Mwanaspoti kuwa amepokea taarifa hizo kwa moyo mkunjufu na atajipanga kuhakikisha anarudi kwenye kikosi cha Stars siku za usoni.


WALA hana nongwa buana! Ndio, beki Abdi Banda anayekipiga Baroka FC ya Afrika Kusini amesema hana kinyongo licha ya kutemwa katika kikosi cha mwisho cha Taifa Stars kitakachoshiriki Fainali za Afcon 2019 zitakazofanyika nchini Misri kuanzia wiki ijayo.

Kutemwa kwa beki huyo wa kati kumezua mijadala kwenye mitandao ya kijamii ambako baadhi ya mashabiki wanaunga mkono hatua hiyo huku wengine wakikosoa.

Hata hivyo, Banda mwenyewe ameliambia Mwanaspoti kuwa amepokea taarifa hizo kwa moyo mkunjufu na atajipanga kuhakikisha anarudi kwenye kikosi cha Stars siku za usoni.

“Nimekubaliana na maamuzi ya benchi la ufundi, kila mtu ana haki ya kuitumikia nchi yake, kama leo nimeachwa mimi basi kesho sitakuwa mimi,” alisema Banda, ambaye pia ni mume wa mdogo wa msanii wa Bongo Fleva, Ali Kiba anayeitwa Zabibu Kiba.

“Kikubwa ninachotaka kusema kwa upande wangu sina wa kumlaumu, nimeheshimu maamuzi maana nina imani kesho nitarudi tena. Hapa si mwisho wa safari.”

Alisema kuwa anarudi kwenye klabu yake kujipanga upya na kuangalia ni wapi hakumridhisha mwalimu ili safari ijayo aweze kuitwa tena akiwa katika kiwango bora zaidi. “Nawapongeza wote waliopata nafasi ya kuiwakilisha nchi na nina imani wataleta heshima tunayoitaka Watanzania,” alimalizia Banda ambaye kabla ya kusajiliwa na Baroka FC alizichezea klabu za Coastal Union na Simba.

Kikosi cha Stars kilichotangazwa na Kocha Emmanuel Amunike kinajumuisha nyota 23 ambao kabla ya kuanza kibarua cha kulitetea taifa wanatarajiwa kukipiga na timu za taifa za Misri na Zimbabwe. Kwa sasa wachezaji hao wapo kambini nchini Misri.