Banda: Njia ya kwenda Afcon ipo Uwanja wa Taifa

Monday September 10 2018

 

BEKI wa kati wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda amesema Taifa Stars inaweza kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Cameroon mwakani kama Watanzania wataendelea kuisapoti timu yao.

Banda alitoa mfano wa namna ambavyo Waganda walivyojitokeza juzi Jumamosi kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Nelson Mandela, Namboole mjini Kampala.

Beki huyo alisema ni vizuri Watanzania kujijengea tabia ya uzalendo ili wachezaji wawe na nguvu ya kulipigania taifa katika mazingira mazuri pindi wanapocheza katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

“Nafasi ya hamasa kwenye mpira ni kubwa, kilichotusaidia Uganda ni ukomavu wetu, ninachoamini kwa sasa Tanzania mbali na kuwa na vipaji, kuna wachezaji wenye ukomavu ambao wanaweza kucheza hata kwenye presha.

“Lakini pia hata ongezeko la wachezaji wanaocheza ligi kubwa naona wanalisaidia taifa letu. Kila Mtanzania anatakiwa kujivunia timu yake ya taifa kwa mwendo huo, tunaweza kufika mbali,” alisema beki huyo.

Hata hivyo, mchezaji huyo wa zamani wa Simba na Coastal Union ya Tanga, alisema kinachoweza kutusaidia kufuzu mwakani kwenye mataifa ya Afrika ni kutumia vyema uwanja wa nyumbani.

Banda alisema inatakiwa tukusanye pointi zote sita za michezo ambayo tutacheza nyumbani ambayo ni dhidi ya Cape Verde,Oktoba 13 mwaka huu na Uganda ambapo itakuwa Machi 22 mwakani.

Kabla ya Taifa Stars kukutana na Cape Verde jijini Dar es Salaam, itacheza nayo mchezo wa kwanza, Oktoba 10 kwao.

Advertisement