Banda, Kichuya, Mkude, Ajibu wajitathimini

Muktasari:

Taifa Stars, ipo nchini Misri kwa ajili ya kucheza michuano ya AFCON, jambo lililomuibua mchambuzi  wa soka nchini, Ally Mayay kusema kitu kuhusiana na mashindano hayo.


MCHAMBUZI  wa soka nchini, Ally Mayay amesema Taifa Stars inaweza kufanya maajabu ya kuiduwaza dunia kwenye michuano ya AFCON inayotarajia kuanza Juni 23 nchini Misri.
Mayay anasema hana mashaka na kikosi ambacho kimechaguliwa  na kocha Emmanuel Amunike akidai kinaendana na falsafa yake ya kucheza mpira wa nguvu na kujilinda.
"Aina ya soka la Amunike ni la kutumia viungo wakabaji wengi na mabeki kitaalamu anataka fitinesi ndio maana nimesema kikosi chake ni sahihi na lazima tuheshimu maamuzi yake"anasema.
Mbali na hili amewageukia wachezaji  waliopata kibali cha kwenda kucheza AFCON, akiwaambia wasimuangushe Amunike na Watanzania kwa ujumla akiwasisitiza wafanye vitu vikubwa ambavyo vitaacha historia kwa ulimwengu mzima.
"Mbali na wachezaji hao kuliwakilisha taifa, lakini ni nafasi nzuri  kwao kupambana na kujipima kwa wachezaji wakubwa ulimwenguni, wanachopaswa kufanya ni kujitambua na watangulize nidhamu ya hali ya juu," anasema Mayay.
Lakini kwa wachezaji ambao wametemwa ndani ya kikosi hicho, amewaambia wasikate tamaa bali wachukulie kama changamoto ya kuongeza bidii na kujisahihisha mapungufu yao.
"Mfano kama Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude, Shiza Kichuya na Abdi Banda bado wana nafasi kubwa ya kulitumikia taifa lao, wasikate tamaa waongeze juhudi ya kufanya viwango vyao viendelee kuwa msaada kwa Tanzania, hivyo kuachwa kwao wajitathimini na wasichukulie kawaida bali iwe kitu cha kuwapa hatua kama wachezaji wenye mtazamo wa kufika mbali"anasema.