Banda: Ajibu inatosha sasa ondoka Yanga!

Muktasari:

  • Mchezaji tegemeo wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda amemwambia mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu wakati wake wa kucheza mpira wa nyumbani umekwisha na sasa afikirie kuondoka kwenda kutafuta changamoto nyingine nje ya nchi.

Dar es Salaam. Kiwango kinachoonyeshwa na mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu kimemfanya beki wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda atamke maneno mazito.

Banda ameguswa kutokana namna anavyomjua mchezaji huyo ndani na nje ya uwanja na hasa baada ya kuanza msimu huu wa Ligi Kuu Bara vizuri akiwa ametengeneza nafasi sita za mabao ya Yanga sambamba na kufunga mawili kati ya 11, waliyonayo mpaka sasa.

Bao hilo la 11, la Yanga lilifungwa na Ajibu na kuwa gumzo kwa wadau wa soka Tanzania kutokana na uhodari aliouonyesha.

Alilifunga akiwa umbali wa takribani mita 16, kutoka golini kwa wapinzani wao, akaruka 'tikitaka' akigeukia upande wa goli lao na kuutia wavuni.

Hiyo ndio ikamfanya, Banda akubali kubeba lawama zote na kueleza kilicho ndani ya moyo wake akisema.

"Kitu kikubwa ambacho naweza kumwambia Ajibu kwa sasa, nadhani muda wake wa kucheza nyumbani umekwisha kwani kila kitu ameshamaliza na sasa atafute changamoto nyingine nje ya Tanzania bila kujali ni Ulaya au sehemu gani,"alisema Banda ambaye wadau wa soka wamekuwa wakimwagia sifa kutokana na mafanikio yake kwenye kikosi cha Baroka.

Banda anasema, anatambua maamuzi hayo ni magumu hasa kutokana na misukosuko ambayo wanakutana nayo nje ya nchi, lakini anachotakiwa kufanya Ajibu ni maandalizi ya kukubaliana na changamoto zote kwani baada ya hapo ni furaha tu.

"Ni kweli kucheza nje si rahisi kihivyo, lakini kitu kikubwa kinachotakiwa ni utayari tu wa kazi hiyo," alifafanua.