Banana Zoro aimwagia misifa Simba

Muktasari:

Timu ya Simba kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo, imemkosha msanii Banana Zoro anayeona timu hiyo levo zake ni za kimataifa na haiwezi kufananishwa na nyingine Ligi Kuu Bara.

MSANII wa bongo fleva, Banana Zoro ameshindwa kuficha furaha yake kutokana na Simba kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu mfululizo,akitamba kuwa levo zao ni za kimataifa.
Simba ilijihakikishia ubingwa huo juzi Jumapili baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Prisons katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya
Matokeo hayo yaliifanya Simba ifikishe pointi 80 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote kati ya zinazoshiriki ligi hiyo.
Staa huyo hajifichi kuwa yeye ni Simba damu,hivyo kitendo cha timu hiyo kuwa mabingwa msimu huu anaona  wao ni wa levo za juu ambazo haziwezi kufanana na timu pinzani.
Amewapongeza wachezaji kwa kujituma kufanikisha malengo ya klabu na furaha ya mashabiki wao,huku akiwataka wajipange vyema ili kuonyesha majabu michuano ya klabu Bingwa Afrika.
"Ujue kila binadamu ana nyakati zake za kufurahi na kuhuzunika, huu ni wakati wa mashabiki wa Simba kutembea kifua mbele kutokana na raha tunayopewa na wachezaji wetu ambao wanapambana kushinda mechi,"
"Wanastahili pongezi kwani sio jambo dogo  kuchukua  ubingwa misimu mitatu mfululizo,hivyo ni zamu yetu kutamba kimataifa, wengine wakisubiri tufanyaje kazi yetu,"amesema.
Amesema anatamani kuona Simba inachukua hadi taji la Kombe la FA ili kuandika historia ya aina yake mwaka huu.
"Kwa kikosi cha Simba kina uwezo wa kufanya lolote ingawa wanacheza na Azam FC ambayo ni timu ngumu ina wachezaji wazoefu,"
"Lakini pia tuwaunge mkono hata Simba Queens na wao wachukue ubingwa ili uwe mwaka wa Simba kwani wakati mkiwa vizuri kiuwezo uwanja ni kufanya kitu cha tofauti,"amesema.