Balinya na Kagere hesabu za kutisha !

Muktasari:

Kwa upande wa Simba bado wanatambia rekodi ya msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakiuwasha moto hadi kutinga hatua ya robo fainali. Kama kawaida, Meddie Kagere (MK14) atakuwa akiongoza jahazi la Msimbazi sambamba na John Bocco.

RATIBA ya Ligi Mabingwa Afrika kwa msimu wa 2019/2020 imetolewa juzi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambapo wawakilishi wanne wa Tanzania Bara, Simba, Yanga, Azam na KMC wote wataanzia hatua ya awali.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba itaanzia ugenini dhidi ya UD Songo ya Msumbiji wakati Yanga itaanzia nyumbani kuikabili Township Rollers ya Botswana.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC itavaana na Fasil Kenema S.C ya Ethiopia na kwa upande mwingine KMC itacheza dhidi ya AS Kigali.

Mechi za kwanza za hatua ya awali zitachezwa kati ya Agosti 9 hadi 11 na zile za marudiano zitachezwa kati ya Agosti 23 hadi 25.

Baadhi ya timu hizo ambazo zimepangwa dhidi ya wawakilishi hao wa Tanzania Bara zinafahamika kwa wapenzi na wadau wa soka nchini, lakini nyingine hazifahamiki.

Kwa kulitambua hilo, makala haya yanakuletea baadhi ya dondoo na taarifa muhimu kuhusiana na wapinzani wa timu za Azam FC, Yanga, KMC na Simba kwenye mashindano ya kimataifa. Mashabiki wa Yanga hawana shaka kutokana na uwepo wa mastaa wapya wakiongozwa na kinara wa mabao wa Ligi Kuu Uganda msimu uliopita, Juma Balinya ambaye ametua kwa wababe wa Jangwani. Mbali na Balinya, pia kuna Maybin Kalengo, Sadney Urikhob, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana ambao wametua kwa ajili ya kurejesha heshima ya Yanga.

Kwa upande wa Simba bado wanatambia rekodi ya msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakiuwasha moto hadi kutinga hatua ya robo fainali. Kama kawaida, Meddie Kagere (MK14) atakuwa akiongoza jahazi la Msimbazi sambamba na John Bocco.

UD SONGO

Mabingwa hao wa Msumbiji mwaka jana, makao yao makuu yapo katika Jiji la Songo Tete, Upande wa Magharibi mwa nchi hiyo, umbali wa kilomita takribani 1650 kutoka Mji Mkuu wa Msumbiji, Maputo

Timu hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Uzalishaji Umeme ya Desportivo iliyopo Magharibi mwa Msumbiji karibu na Mto Zambezi na Bwawa la Cahora Bassa na imeanzishwa mwaka 1982 ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya mara mbili.

Mafanikio yake makubwa ni kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018 ambapo ilishika nafasi ya tatu ikimaliza na pointi tatu ambazo zote ilizipata kwa sare huku ikipoteza mechi tatu.

Ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Msumbiji kwa mara mbili mfululizo, 2017 na 2018.

Nyota tegemeo wa Songo ni Helder Pelembe anayecheza nafasi ya ushambuliaji na kipa Leonel ambaye ndiye chaguo la kwanza kwenye Timu ya Taifa ya Msumbiji na inafundishwa na mchezaji nyota wa zamani wa nchi hiyo Nacir Armando.

Katika mechi 10 za mwisho za mashindano ya kimataifa, imepata ushindi mara moja, imetoka sare tatu na kupoteza mechi sita.

TOWNSHIP ROLLERS

Ni mara ya pili kwa Yanga kukutana na Township Rollers kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mara ya kwanza ikiwa ni 2018 zilipoumana katika hatua ya kwanza ambapo wawakilishi hao wa Tanzania waliondolewa kwa matokeo ya jumla ya kipigo cha mabao 2-1, wakifungwa nyumbani na kutoka sare ugenini.

Timu hiyo ambayo ni mabingwa wa taji la Ligi Kuu ya Botswana kwa misimu minne mfululizo kuanzia ule wa 2015–16 hadi uliomalizika wa 2018/2019, ilianzishwa mwaka 1961 ikitumia Uwanja wa Taifa Botswana ambao unaingiza takribani mashabiki 25,000, kwa ajili ya mechi zake za nyumbani za mashindano ya kimataifa.

Ni timu iliyofanikiwa zaidi Botswana kwani imetwaa Ligi Kuu mara 15, Kombe la FA mara sita, lakini pia imetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja. Makao Makuu yake yapo Gaborone, Botswana na nyota wake tegemeo ni kipa Keagile Kgosipula, viungo Ivan Ntege, Lemponye Tshireletso na washambuliaji Segolame Boy na Joel Mogorosi na kocha wao ni Tomas Trucha kutoka Czech.

FASIL KENEMA

Wahabeshi wamepangwa na Azam FC hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la FA. Tangu ilipoanzishwa mwaka 1960 hadi sasa haijawahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya kwao na mafanikio yake makubwa ni kutwaa Kombe la FA ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa.

Inafundishwa na kocha mzawa, Webetu Abate na wachezaji wao tegemeo ni beki na nahodha, Amsalu Tilahun huku straika akiwa ni Abdurahiman Mubarek. Timu hiyo ipo kwenye Mji wa Gondar uliopo Kaskazini mwa Ethiopia na inatumia Uwanja wa Fasiledes unaoingiza mashabiki 20,000.

AS KIGALI

Baada ya kuishtua Rwanda kwa kuwachapa mabingwa wa Ligi Kuu wa nchi hiyo, Rayon Sports kwenye Kombe la Kagame, wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, KMC wamerudishwa tena nchini humo ambako watapambana na AS Kigali kwenye hatua ya awali.

Timu hiyo iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda msimu wa 2017/2018 na Kombe la FA nchi hiyo msimu uliopita, inautumia Uwanja wa Amahoro unaoingiza takribani mashabiki 30,000 ambao upo Kigali kwa mechi zake za nyumbani.

AS Kigali inanolewa na nyota wa zamani wa Timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, Eric Nshimiyimana ambaye amerejea klabuni kuziba nafasi iliyoachwa na kocha wa zamani wa Simba, Masoud Djuma ambaye alitimuliwa kutokana na matokeo mabovu ya timu hiyo msimu uliopita. Wachezaji wake tegemeo ni nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Haruna Niyonzima na aliyekuwa beki wa Singida United, Michel Rusheshangoga.

Maoni ya wadau

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Ng’ambi alisema timu waliyopangwa nayo sio ya kubeza na watajipanga kuhakikisha wanavuka kwenda hatua za juu.

“Songo ni timu nzuri na nimeiona iliwahi kuifunga TP Mazembe, hivyo hatuwezi kuidharau. Kikubwa tunaendelea na maandalizi ili tuweze kufanya vizuri lakini jambo lenye faida kwetu ni kwamba tumefanya usajili wa kikosi kizuri na kipana ambacho kinaweza kuhimili ratiba iliyo mbele yetu,” alisema Nghambi.

Mratibu wa Azam FC, Phillip Alando alisema wanaspwa kujiandaa ili kukabiliana na ratiba hiyo ambayo imekuja kinyume cha matarajio.

“Kwa mtazamo wangu ninaona kama ni ratiba ya kushtukiza kwa kuwa timu zetu hazikuzoea mashindano haya kuchezwa katika tarehe hizi zilizotajwa.