Bale akubali yaishe kwa Zidane

Muktasari:

Kwa sasa Bale, mchezaji anayelipwa Pauni 600,000 kwa wiki amekubali yaishe wakati mkataba wake ukielekea ukingoni kuelekea mwaka 2022 ili aweze kuongezewa mkataba mwingine klabuni hapo.

MADRID, HISPANIA . MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Gareth Bale yupo tayari kuondoa kinyongo dhidi ya kocha wake, Zinedine Zidane ili kurejesha uhusiano wao vizuri, ambapo amepanga kupigania namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Bale na Zidane walitofautiana msimu uliopita kocha huyo alipoanza kumuweka benchi mchezaji huyo na kumlazimu kuanza kusaka timu ya kuhamia, jambo lililomfanya kuhusishwa na timu nyingi ikiwamo zile za China. Hata hivyo, mabosi wa Real walizima mpango wake wa kuhama baada ya majeruhi kuongezeka katika timu hiyo.

Tangu wakati huo mchezaji huyo na kocha wake wamekuwa wakiishi bila uhusiano wa karibu ‘wa kocha na mchezaji’, ikielezwa kwamba umeathiri kwa kiasi kikubwa kiwango cha Bale ambacho kimeporomoka zaidi na hivyo kumuondoa kabisa katika kikosi cha kwanza cha wababe hao wa Santiago Bernabeu.

Kwa sasa Bale, mchezaji anayelipwa Pauni 600,000 kwa wiki amekubali yaishe wakati mkataba wake ukielekea ukingoni kuelekea mwaka 2022 ili aweze kuongezewa mkataba mwingine klabuni hapo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Mirror la Uingereza, mchezaji huyo amekuwa akifanya

‘mawasiliano ya kirafiki’ na Zidane katika juhudi zake za kutaka kumsogeza karibu kocha huyo ili

aendeleze kipaji chake ndani ya kikosi cha kocha huyo Mfaransa.

Hata hivyo, habari iliyochapishwa katika jarida la Diario la Hispania ilisema juzi kuwa, ifikapo Juni 30, mikataba ya wachezaji 37 klabuni hapo itahitaji kujadiliwa upya na huenda Bale aliyeifungia Real mabao 80 katika mechi 169 akaingia katika kundi hilo linalohusisha nyota wa kikosi cha kwanza, pili, tatu na vile vya vijana wa umri tofauti.

Vyombo vya habari vya Uingereza vimekuwa vikimhusisha mchezaji huyo kurejea katika timu yake ya zamani ya Tottenham, Hotspur, lakini pia Manchester United, Chelsea na klabu za Italia na China zimeendelea kumtolea macho mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales, hivyo lolote linaweza kutokea katika dirisha lijalo na usajili.