Bale aifagilia Tottenham Spurs kumchukua Mourinho

Muktasari:

Kutokana na hilo watu wamekuwa wakiamini kwamba kuna uwezekano Bale akafungulia milango ya kurudi Spurs hasa kwa kipindi hiki mambo yake yakiwa magumu huko Real Madrid, ambako hakubaliki sana.

LONDON, ENGLAND.VIPI anataka kurudi? Staa wa Real Madrid, Gareth Bale ameibua uvumi kwamba huenda anataka kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Tottenham Hotspur baada ya kusifia timu hiyo kwa uamuzi wa kumchukua kocha Jose Mourinho.

Mourinho alichaguliwa kuwa kocha wa Spurs wiki mbili zilizopita baada ya Mauricio Pochettino kufutwa kazi kufuatia kuinoa timu hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

"Kuwa na Jose Mourinho kwenye timu huo ni ujumbe maalumu kutoka kwa timu, nadhani ni kocha wa ushindi," alisema Bale.

"Tottenham wanataka kushinda mataji na sidhani kama kutakuwa na muunganiko mzuri zaidi ya Mourinho na Tottenham wakijaribu kuwa pamoja kubeba mataji."

Kutokana na hilo watu wamekuwa wakiamini kwamba kuna uwezekano Bale akafungulia milango ya kurudi Spurs hasa kwa kipindi hiki mambo yake yakiwa magumu huko Real Madrid, ambako hakubaliki sana.

Mara kadhaa Bale amekuwa akikutana na wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wa Los Blancos wakimzomea licha ya kufanya mambo kadhaa matamu kwenye kikosi chao.