Balaa la Mugalu, Lamine na Mwamnyeto kazi wanayo

KASI ya upachikaji mabao ya Chris Mugalu ndani ya kikosi cha Simba imeanza kuwa gumzo kuelekea mechi ya watani Novemba 7  pale Uwanja wa Mkapa, Dar.

Kama ilivyo ubora wa ukuta wa Yanga, wadau wa soka hususan wa Simba wamekuwa wakitambia ubora wa straika huyo ambaye amekuwa na rekodi za ufanisi wa aina yake katika siku za hivi karibuni licha muda mchache aliopata kikosini Simba.

Mshambuliaji huyo licha ya kucheza katika mechi tatu tu za ligi, amefunga mabao matatu ambayo ni wastani wa bao moja katika kila mchezo jambo ambalo Simba wameanza kutamba atawainua kwenye mechi ijayo na Yanga.

Ukiondoa hayo matatu ya ligi, Mugalu ameichezea pia Simba mechi mbili za kirafiki dhidi ya Vital’O ya Burundi na African Lyon na kuifungia mabao mawili, moja katika kila mchezo.

Hata hivyo, wakati wengi wakishangazwa na kasi ya Mugalu kufumania nyavu, Mwanaspoti limebaini siri mbili ambazo ziko nyuma ya mabao ya mshambuliaji huyo raia wa DR Congo.

Jambo la kwanza ni kuwa nyota huyo anahitaji dakika 15 za kuwepo uwanjani kwenye mechi yoyote ya mashindano ili apachike bao tofauti na mastraika wengine ndani ya kikosi cha timu yake na hata nyingine.

Ukiondoa mechi ya kwanza aliyofunga ambayo ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Vital’O aliyotumia dakika 32 za uwepo wake uwanjani na ile ya kirafiki dhidi ya African Lyon aliyotumia dakika 46, mechi nyingine zote zilizofuata amehitaji angalau muda wa robo saa tu kuweza kuzitingisha nyavu za timu pinzani.

Katika mchezo dhidi ya Biashara United ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Mugalu alitumia dakika nane (8) tu kufunga bao baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi na aliingia dakika ya 76 na kufumania nyavu dakika ya 84.

Ukiondoa hiyo, Mugalu alikuja kufunga tena katika dhidi ya Gwambina na alitumia dakika 15 tu kufunga bao baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi, akichukua nafasi ya Meddie Kagere dakika ya 75 na kufunga bao lake dakika za nyongeza.

Juzi Jumapili katika mechi dhidi ya JKT Tanzania, mshambuliaji huyo alihitaji dakika tisa tu za uwepo uwanjani, kupachika bao na alianza kikosini na kufunga bao lake dakika ya tisa ya mchezo akiunganisha kwa kichwa krosi ya Luis Miquissone.

Jambo la pili ambalo limebainika kwa mabao hayo ya Mugalu ni staili yake ya ufungaji na amekuwa akifanya hivyo huku akiwa analitazama lango pasipo bugudha ya mabeki wa timu pinzani na amekuwa akitumia zaidi mguu wa kushoto.

Uwezo wa kujipanga na kuwahi kufika katika nafasi sahihi na utulivu wake mbele ya lango, umesababisha Mugalu kuonekana akifunga mabao mepesi ambayo ameyapata pasipo kubanwa na mabeki wa timu pinzani baada ya kupokea mpira akiwa huru.

Kati ya mabao hayo matano aliyofunga, manne ameyafunga kwa kutumia mguu wake wa kushoto huku moja akifunga kwa kichwa.

Pasi zinazotokea katikati na kushoto ndizo zinaonekana kuzalisha idadi kubwa ya mabao ya Mugalu kwani amefunga mabao mawili kutokana na pasi zilizotokea eneo hilo huku mengine mawili yakitokana na pasi ya upande wa kushoto na lingine kutokea upande wa kulia.

Katika kudhihirisha wachezaji wa Simba wamefahamu mapema namna ya kumchezesha Mugalu, mabao yote matano aliyofunga yametokana na pasi za mwisho kutoka kwa wachezaji watano tofauti.

Bao dhidi ya Vital’O lilitokana na pasi ya Miraji Athuman na katika mechi dhidi ya Biashara United, alipokea pasi ya Clatous Chama huku katika mechi dhidi ya African Lyon akifunga kutokana na pasi ya Ibrahim Ajibu.

Katika mchezo dhidi ya Gwambina, bao lake lilitokana na pasi ya Bernard Morrison na kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania, pasi ya mwisho iliyopigwa na Luis Miquissone ndio aliyoitumia kupatia bao lake.

Akizungumzia makali ya Chris Mugalu, mchambuzi wa soka na mchezaji wa zamani wa Kariakoo Lindi, Jemedari Said alisema;

“Kikawaida hakuna mchezaji anayependa kuanzia benchi hivyo hata huyo Mugalu anaweza kuonekana kama mchezaji hatari hasa akitokea benchi na Simba wakajiaminisha hivyo lakini bila shaka moyoni mwake nia yake ni kuwa anaanza katika kikosi cha kwanza.”

“Hivyo kwa vile anafanya vizuri, benchi la ufundi linatakiwa kumpa nafasi ya kucheza na iwapo akishindwa kuwa na ufanisi ndipo mambo yawe tofauti. Mchezaji kama yeye anafanya akina Meddie Kagere na John Bocco kuimarika na kujituma zaidi kwa sababu wanafahamu wakishindwa kufanya vizuri atawapora nafasi,” alisema Jemedari.

Kocha wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije alisema aliwahi kupata nafasi ya kwenda kuangalia mazoezi ya Simba na kumwona Mugalu kila krosi ambayo inapigwa anafunga.

Ndayiragije alisema bao ambalo alifunga Mugalu katika mechi na JKT Tanzania alikuwa kama mchezaji asiyekuwa na madhara aliinama kwanza na wakati krosi inakaribia kufika aliruka kichwa katikati ya mabeki wawili akiwa huru baada ya kuwazuga na akafunga.

“Ukiangalia aina ya bao alilolifunga Mugalu na JKT linataka kufanana na lile la pili ambalo alifunga Mbwana Samatta akiwa na timu yake mpya Fenerbahce.

“Naiona Simba itakuwa ikifunga mabao mengi wanapokuwepo mastraika wawili katika kikosi cha kwanza na nilitegemea hilo baada ya kuwaona Mugalu na Kagere katika mechi ya JKT Tanzania na kweli yakatokea,” alisema Ndayiragije ambaye kikosi chake kipo kambini kujiandaa na mechi ya Burundi Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa.