Balaa la Cavani, Kane na Mo Salah wajipange tu

LONDON, ENGLAND. UMEMWONA Edinson Cavani? Anapiga tizi la kutosha kivyake akiwa amejitenga kama kanuni ya janga la virusi vya corona inavyohitaji baada ya kunaswa na Manchester United.

Straika huyo wa kimataifa wa Uruguay, Cavani, 33, alituma video yake Instagram akipiga tizi kali kujiweka fiti huku akiwa na uzi wa mazoezi wa Man United.

Cavani alisaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine zaidi huko Man United wenye thamani ya Pauni 200,000 kwa wiki. Lakini, sasa baada ya kuwasili kutoka Ufaransa, atalazimika kujifungia kwa siku 14 kutokana na kanuni za corona. Kama mambo yatakuwa hivyo, Cavani hatacheza dhidi ya Newcastle United, Oktoba 17 na atakuwa na siku moja tu ya kujiunga na wenzake kabla ya kuwakabili timu yake ya zamani Paris Saint-Germain.

Unaambiwa hivi, Cavani ni balaa jingine linapokuja suala la kufunga. Tangu aanze kucheza soka, wachezaji wanaomzidi kwa mabao ni wawili tu, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Zaidi ya hapo, atatua Ligi Kuu England ambako hakuna straika yeyote anayeweza kumshinda kwenye kufunga kuanzia Harry Kane wa Tottenham, Sergio Aguero wa Manchester City, Mohamed Salah wa Liverpool, Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal na hata Jamie Vardy wa Leicester City hawatii mguu kwa fowadi huyo matata.

Katika Ligi Kuu tano bora za Ulaya, kuanzia Machi 11 2007, ni Ronaldo na Messi pekee yake ndio wanaomzidi Cavani kwa mabao, ambapo ndani ya muda huo, ametikisa nyavu mara 250. Anashika namba tatu kwa mabao nyuma ya Ronaldo na Messi. Ronaldo anayekipiga Juventus kwa sasa amefunga mabao 416, wakati staa wa Barcelona, Messi amefunga mabao 432. Cavani alihitaji mechi 413 kufunga mabao 250, wakati Ronaldo mabao yake aliyofunga alihitaji mechi 433 na Messi mechi 450. Amepita kwenye timu za Palermo, Napoli na PSG kabla ya sasa kutua Man United, huku akifunika mastraika wote waliopo Ligi Kuu England.

Ndani ya muda huo, Aguero amejaribu kufurukuta akifunga mabao 248 na walau anamkaribia Cavani kwa mastaa waliopo Ligi Kuu England kwa sasa. Aguero amecheza idadi sawa ya mechi na Cavani, ila anazidiwa mabao mawili. Tano bora ya mastaa waliotikisa nyavu mara nyingi kwenye Ligi Kuu tano bora za Ulaya kwa kuanzia Mei 11, 2007 inakamilishwa na Zlatan Ibrahimovic, mwenye mabao 245 katika mechi 330. Mabao yake mengi Cavani alifunga akiwa na kikosi cha PSG.

Alifunga mabao 138 katika mechi 200. Kwenye kikosi cha Napoli kwanza alipocheza kwa mkopo akitokea Palermo alifunga mabao 26 katika mechi 35 na baada ya kubeba jumla, alifunga mabao 52 katika mechi 69 kabla ya kusajiliwa na PSG. Kwenye kikosi cha Palermo alifunga mabao 34 katika mechi 109.