Balaa Kubwa

Muktasari:

Wikiendi ya kwanza ya ligi hiyo ilishuhudia wababe wa Big Six, Manchester United wakimenyana na Chelsea na wikiendi hii ya pili ni Man City na Spurs, ni balaa kubwa.

LONDON,ENGLAND.KOCHA Unai Emery bila shaka atafunga mziki mnene wa kikosi chake cha Arsenal kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Burnley huko Emirates ili kuhakikisha anaketi pale juu kwenye msimamo wa ligi hiyo. Arsenal itakipiga na Burnley mapema kabisa na Kocha Emery anafahamu wazi hiyo ni fursa ya kuketi kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo leo Jumamosi.

Hadi sasa Arsenal imeshakusanya pointi tatu baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle United kwenye mchezo uliopita, hivyo ushindi dhidi ya Burnley utaiweka kileleni hadi hapo baadaye, wakati Manchester City itakapokipiga na Tottenham uwanjani Etihad, lakini hilo litategemea matokeo.

Katika mchezo huo, Emery anatazamiwa kuanzisha safu yake matata ya ushambuliaji, itakayoundwa na Nicolas Pepe, Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette, kitu ambacho mashabiki wa wababe hao wa Emirates wanasubiri kwa hamu sana kuona wakali hao watakapocheza pamoja, wapinzani watateseka kiasi gani ndani ya uwanja. Hilo linasubiriwa kwa hamu huko Emirates.

Mchezo huo pia unaweza kumshuhudia beki David Luiz akicheza mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa Arsenal baada ya kutua kwenye timu hiyo akitokea Chelsea kwa ada ya Pauni 8 milioni.

Mechi kali zaidi ya leo itakuwa huko Etihad, wakati Pep Guardiola na chama lake la Man City atakapomkaribisha Mauricio Pochettino na Spurs yake katika mechi ngumu inayotazamiwa kuwa na mvuto mkubwa kutokana na kuhusisha wakali wa Big Six.

Wikiendi ya kwanza ya ligi hiyo ilishuhudia wababe wa Big Six, Manchester United wakimenyana na Chelsea na wikiendi hii ya pili ni Man City na Spurs, ni balaa kubwa.

Katika mchezo wa kwanza, Man City iliichapa West Ham United 5-0, wakati Spurs yenyewe ikiichapa Aston Villa 3-1. Katika mechi hizo, Raheem Sterling alipiga hat-trick upande wa Man City, wakati huko kwingine Harry Kane alipiga mbili upande wa Spurs. Usiku wa leo watamalizana wenyewe kwa wenyewe.

Hata hivyo, kutakuwa na mechi nyingine, ambapo Liverpool ikitokea kusherehekea ubingwa wa Uefa Super Cup, itakwenda ugenini kwa Southampton huko St Mary’s huku ikiwa na kumbukumbu ya kushinda 4-1 dhidi ya Norwich City kwenye mechi yake ya kwanza na Kocha Jurgen Klopp atahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuendelea kukimbizana na wapinzani wake kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Aston Villa itapata nafasi ya kujiuliza mbele ya Bournemouth, huku Everton ikiwa na shughuli pevu mbele ya Watford.

Norwich City baada ya kupoteza mechi ya kwanza, itakuwa nyumbani kuikaribisha Newcastle, ambao pia inamajeruhi ya kupigwa kwenye mechi yake ya kwanza, huku Brighton ikiikaribisha West Ham iliyotoka kupigwa Tano Bila kwenye mechi yao ya ufunguzi kwenye ligi.

Mchakamchaka wa ligi hiyo utaendelea kesho Jumapili kwa mechi mbili tu, ambapo Sheffield United itakuwa nyumbani kuikaribisha Crystal Palace ya staa Wilfried Zaha, huku Chelsea ikitokea kwenye kichapo cha Nne Bila itakuwa nyumbani Stamford Bridge kukipiga na Leicester City.

Mchezo huo utakuwa mtihani kwa Kocha Frank Lampard akisaka ushindi wake wa kwanza kwenye mechi ya kiushandani tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo ya Stamford Bridge kutoka kwa Maurizio Sarri. Jumatatu usiku kutakuwa na mechi moja tu, Manchester United itakwenda ugenini kuifuata Wolves, ambayo mara nyingi imekuwa ikiteseka sana inapokabiliana nayo.

Msimu uliopita, Man United ilichezea vichapo mara nyingi kwenye mechi dhidi ya Wolves, huku itakwenda katika mechi hiyo, ikiwakuta wenyeji wao kwenye mzuka mkubwa baada ya kupiga mtu Nane Bila kwenye mechi mbili za kufuzu mikikimikiki ya Europa League dhidi ya Pyunik.