Bakayoko kakiwasha,Gattuso akubali mavitu

Muktasari:

  • Bakayoko ametua Milan kwa mkopo akitokea Chelsea na mwanzoni maisha yake yalikuwa magumu kabla ya staa huyo wa Ufaransa kubadili hali ya mambo na kuuwasha moto huko San Siro.

MILAN, ITALIA.TIEMOUE Bakayoko ghafla tu amebadili upepo huko AC Milan na kumfanya Kocha Gennaro Gattuso kumtaka asaini dili la moja kwa moja wakati mkopo wake utakapofika tamati mwisho wa msimu.

Bakayoko ametua Milan kwa mkopo akitokea Chelsea na mwanzoni maisha yake yalikuwa magumu kabla ya staa huyo wa Ufaransa kubadili hali ya mambo na kuuwasha moto huko San Siro.

Kiwango chake bora sasa kimemkosha Kocha Gattuso na kudai atapenda kuona kiungo huyo atasaini dili la moja kwa moja la kuitumikia timu hiyo kwenye Serie A. Huduma ya Bakayoko inaweza kupatikana kwa dau la Euro 35 milioni.

“Tutaweza kulipia kiwango kilichowekwa kwenye mkataba wa Bakayoko? Mimi si mhusika wa jambo hilo,” alisema Gattuso.

“Kilichopo, tutatafuta pesa ya kufanya hivyo. Kitu ambacho nakifanya kwa sasa ni kumfanya awe na kiwango bora tu ndani ya uwanja. Viongozi wao watafahamu kitu gani cha kufanya na ni pesa kiasi gani inafaa kutumika ili kumnasa mchezaji huyu, kwa kuwa anatufaa,” alisema.