Babu amuondoa Ngassa kambini Moro

Muktasari:

Amesema mazoezi hayo yanafanyika kwa weledi mkubwa na muitikio wa wachezaji waliojiunga mpaka sasa ni mkubwa chini ya makocha Noel Mwandila na Peter Manyika.

WINGA mkongwe Mrisho Ngassa amelazimika kuondoka kambini mkoani Morogoro baada ya kupata msiba wa babu yake, taarifa ya klabu hiyo imetolewa.
Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh amesema Ngassa alijiunga kwa wakati kambini lakini amelazimika kuondoka baada ya kupata msiba wa babu yake mzaa mama.
Hafidh amesema mkongwe huyo atarejea haraka kuendelea na mazoezi hayo baada ya kumaliza mchakato wa msiba huo uliotokea mjini Shinyanga.
Hafidh amesema mpaka sasa hakuna majeruhi yoyote katika kambi yao na mambo yanaendelea vizuri wachezaji kujifua kwa mazoezi makali.
Amesema mazoezi hayo yanafanyika kwa weledi mkubwa na muitikio wa wachezaji waliojiunga mpaka sasa ni mkubwa chini ya makocha Noel Mwandila na Peter Manyika.
Aidha Hafidh amesema wachezaji ambao hawajajiunga na kambi hiyo mpaka sasa wengi wataanza kujiunga kesho Jumapili kama ambavyo ratiba ya ruhusa yao inavyoonyesha.