Baba wa Kompany ashinda, awa meya wa kwanza mweusi Ubelgiji

Muktasari:

Hatimaye Pierre Kompany ambaye ni baba mzazi wa nahodha wa Manchester City na beki wa Ubelgiji, Vincent Kompany ameandika historia katika siasa baada ya kuchaguliwa kuwa Meya wa kwanza mweusi nchini Ubelgiji, akishinda kiti cha kitongoji cha Ganshoren, Brussels.

Brussels, Ubelgiji. Baba wa beki mahiri wa ambaye ni nahodha wa Manchester City, Vincent Kompany, ameandika historia baada ya kuwa Meya wa kwanza mweusi nchini Ubelgiji.

Baba huyo Pierre Kompany, aliyezaliwa mjini Bukavu, DR Congo, Septemba 8, 1947, amechaguliwa kuwa Meya wa kitongoji cha Ganshoren mjini Brussels, Ubelgiji.

Kompany aliwasili Ubelgiji mwaka 1975 akiwa mkimbizi kutoka DR Congo na baada ya kuzoea mazingira alijitosa kwenye siasa za Ubelgiji mwaka 2006 akiwa Kansela na baadaye mwaka 2014 akatwaa kiti cha ubunge wa Mkoa wa Brussels.

Hata hivyo inaaminika kuwa umaarufu wake umechangiwa zaidi na umahiri watoto wake kwa usakataji kabumbu kwani mbali ya Vincent Kompany anayekipiga City na timu ya Taifa ya Ubelgiji pia mwanae Francois, anaichezea timu ya KSV Roeselare ya Ligi Kuu Ubelgiji.

Mara baada ya kutangazwa mshindi wa kiti hicho, watoto wake wote walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumtumia salamu za pongezi kupitia mtandao wa Instagram, ambapo Vincent pekee anao wafuasi 1.6 milioni kwenye mtandao huo.