Baba wa Ali Kiba afariki dunia, kuzikwa makaburi ya Kisutu leo

Muktasari:

Baba wa msanii Alikiba amefariki dunia leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu tangu Desemba 27 mwaka jana.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Ali Kiba amefiwa na baba yake Saleh Kiba leo katika Hospitali ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa takribani siku 21 na maziko yanatarajiwa kufanyika leo Alhamisi.

Akithibisha taarifa ya kifo hicho, Abdu Kiba ambaye ni mdogo wa Ali Kiba alisema ni kweli baba yao amefariki na msiba upo nyumbani kwao Kariakoo Mtaa wa Muheza.

Abdu Kiba amesema baba yao anatarajiwa kuzikwa leo Alhamisi saa 10:00 jioni katika makaburi ya Kisutu na ataswaliwa Msikiti wa Madina uliopo  Karikaoo, jijini Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Neema Mwangomo amesema Mzee Saleh, alifikwa na mauti leo saa 12:05 katika hospitali hiyo.

Neema alibainisha kwamba baba huyo alifikishwa hospitalini hapo tangu Desemba 27 mwaka jana.