Baada ya miaka 15 Simba yarudi Musoma, Stam kikwazo

Thursday April 25 2019

 

By Masoud Masasi

Mwanza. Huko mkoani Mara kwa sasa ni shangwe tu unaambiwa baada ya takribani miaka 15 hatimaye watakosha macho yao kwa kuwaona Simba katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa kwenye uwanja wa Karume dhidi ya wenyeji Biashara United.

Tangu Polisi Mara imeshuka Daraja Msimu wa 2003/04 Simba hawakuwahi kufika mkoani humo jambo ambalo lilifanya mashabiki wa soka kuishia kuwaona wachezaji kwenye luninga na kuwasoma kwenye magazeti.

Afisa Habari wa klabu ya Biashara United, Shomari Binda alisema maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika ambapo amewataka mashabiki wa soka kuja kwa wingi kwenye mchezo huo wa kwanza baada ya miaka 15 iliyopita.

“Tumewaletea burudani hapa Musoma mashabiki waje kwa wingi kutazama huu mchezo ili wawape sapoti wachezaji wetu wa Biashara United”alisema Binda.

Kocha wa Biashara United, Amri Said ‘Stam’alisema wala hana presha kuelekea mchezo huo kesho jumapili dhidi ya Simba ambapo amewataka mashabiki wa timu hiyo kujaza uwanja wa Karume ili kuwapa sapoti.

Alisema vijana wake wapo fiti kuwakabili Simba katika mchezo huo ambao ni muhimu sana kwao kuweza kupata ushindi ambao utawafanya watoke mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Advertisement

Stam alisema anawajua sehemu ya kuwathibiti Simba kwani msimu huu alishawafunga wakati anakinoa kikosi cha Mbao FC.

“Tunahitaji ushindi ambao utatufanya tufikishe pointi 37 ambazo angalau zitatuweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa Ligi,”alisema Stam.

Advertisement