Baada ya kipigo CAF yaikubalia Al Ahly, Sundowns kurudi kuchezwa Uwanja wa Borg El-Arab

Muktasari:

  • Sundowns ilichapa Ahly mabao 5-0 katika mchezo wa kwanza na kuiweka katika mazingira magumu miamba hiyo ya Cairo katika jitihada zake za kusaka ubingwa wa tisa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Cairo, Misri. Pamoja na awali kukataa, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limebadili uamuzi na kuiruhusu Al Ahly itakayokuwa mwenyeji wa Mamelodi Sundowns katika mchezo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kutumia uwanja wa Borg El-Arab, Alexandria Jumamosi ijayo.

Al Ahly watakuwa wenyeji wa mabingwa wa Afrika Kusini huku wakiwa na kumbukumbu ya kupokea kipigo cha mabao 5-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Afrika Kusini.

CAF hivi karibuni ilitangaza kuzuia kutumika kwa uwanja huo baada ya sehemu ya kuchezea ya uwanja wa Borg El-Arab kuwa katika hali mbaya kutokana na kuchezewa kwa michezo mingi ya ligi na mashindano ya kimataifa.

Hata hivyo, Ahly imesisitiza kutaka kucheza mechi yake ya Jumamosi kwenye uwanja wa mjini Alexandria ambako mechi zake zote za mashindano msimu huu zimechezwa hapo pia imekuwa na mashabiki wengi.

Ahly iliyofuzu kwa fainali mara mbili mfululizo na kukosa ubingwa wanahitaji mujiza katika mchezo wao wa marudiano ili kusonga mbele.