BUKU 20 TU, Simba SC yaunasa mtambo wa mabao

Wednesday May 20 2020

 

By IMANI MAKONGORO

NI miaka 22 sasa imepita tangu mshambuliaji, Athuman Machupa aliposajiliwa kwa mara ya kwanza kukipiga kwenye kikosi cha wababe wa Msimbazi, Simba.

Machupa alisajiliwa Simba mwishoni mwa mwaka 1998 akitokea Malindi ya Zanzibar ambako alikuwa akiuwasha moto na ghafla jina lake likasikika Bara na watu wenye pesa zao wakaanza harakati za kusaka saini yake.

Lakini, utamu ni namna alivyonaswa na Simba kuanzia hatua ya kwanza hadi anakabidhiwa jezi ya Wekundu hao wa Msimbazi.

“Niliitwa kwenye majaribio nikafanya vizuri, nikapewa fomu maalumu ya kujaza na hapo nikaambiwa kwamba, tayari ni mchezaji wa Simba,” anaanza kusimulia Machupa.

Safari yake ilianzia Magomeni

Machupa anakumbuka alivyosajiliwa Simba akiwa kijana mdogo, ambaye alianza safari yake ya soka kwenye timu za mtaani maarufu kama Chandimu.

Advertisement

“Wakati huo nilikuwa nikisoma shule ya msingi Uhuru, timu yangu ya utoto ilikuwa Garden FC ya Magomeni, kabla ya kuchukuliwa na Friends Rangers,” anasimulia.

Anasema katika maisha yake ya soka, Friends Rangers ndiyo timu ambayo ilimjenga hadi kusajiliwa kwenye kikosi cha Malindi ambako, alicheza msimu mmoja na Simba kumchukua.

Usajili wake Simba ulikuwa hivi

Machupa anasema aliitwa kwenye majaribio baada ya kumaliza mkataba wake Malindi, ambayo alifuzu na kuchukuliwa kwenye kikosi hicho.

“Katika usajili wangu, nilipewa bahasha ndani ilikuwa na Sh20,000 na makubaliano ya kulipwa mshahara wa Sh60,000 kwa mwezi,” anasimulia Machupa.

Anasema wakati ule aliona fahari tu kucheza Simba, hivyo hakuangalia pesa ngapi anapewa ingawa kwa kipaji chake, ingekuwa sasa angeingiza mamilioni ya pesa.

“Unajua wakati ule kuvaa tu jezi ya Simba ilikuwa fahari kwa kijana aliyezaliwa Dar es Salaam, unaona kama unachezea timu ya nyumbani, hivyo kitendo cha kupata nafasi hiyo kwangu ilikuwa ni hatua kubwa mno kuliko hata fedha niliyopewa wakati ule,” anasimulia.

Anasema alicheza Simba kwa mafanikio makubwa, ingawa mara kadhaa Yanga walimshawishi kuikacha timu hiyo na kujiunga Yanga.

“Si chini ya mara tatu Yanga walinifuata, lakini pesa ambayo walikuwa wakinitajia kama ofa yao ilikuwa haifikii hata nusu ya niliyokuwa nikipata Simba, ndiyo sababu niliwapotezea,” anasimulia.

Anasema licha ya Simba kumpa mshahara mdogo, lakini alikuwa na watu ambao walimpa pesa nje ya mshahara, jambo ambalo aliamini akienda Yanga hawezi kukutana nalo.

Alivyowahadaa Yanga

Katika mechi za watu imezoeleka zina mambo mengi ikiwamo ya kishirikina, jambo ambalo Machupa anasema akiwa Simba walitumia mbinu ya kuwachota akili wapinzani wao Yanga kuwa wameshiriki matukio hayo.

“Nimecheza mechi za Simba na Yanga kama nane au 10 nikiwa Simba, hizi mechi buana zina mambo mengi, nakumbuka tuliwahi kuruka ukuta kuingia uwanjani ili kuwapumbaza Yanga,” anasimulia.

Anasema wakati akicheza Simba, makocha waliokuwepo hawakuwa na mambo ya kuamini ushirikina na mpira, hivyo vitendo hivyo kwa wachezaji havikufanyika.

“Sasa ikitokea mechi ya Simba na Yanga, baadhi walikuwa wakiamini lazima mambo hayo yafanyike tena kwa pande zote mbili, tulichokuwa tunafanya ni kuibuka na tukio la ajabu tu uwanjani ambalo litawaaminisha wapinzani wetu ni masharti ya kiganga, lakini hakuna lolote.

“Kuna moja ilitokea tuliruka ukuta kuingia uwanjani, ile ilikuwa ni mbwembwe tu na Yanga ikawavuruga kisaikolojia,” anasimulia.

Machupa anasema tukio ambalo hawezi kulisahau kwenye mechi za watani ni lile alilopewa kadi nyekundu.

“Sikumbuki ilikuwa mwaka gani, lakini nilifunga bao katika mechi hiyo na ndiyo lilikuwa bao langu la kwanza kuifunga Yanga, wakati huo kulikuwa na maneno maneno ya mashabiki wa Yanga.

“Nilifunga dakika za lala salama, bao ambalo liliwafunga midomo Yanga, nilifurahi kupitiliza nikajikuta nashangilia ndivyo sivyo hadi kupewa kadi nyekundu, hata hivyo kadi ile haikuchukuliwa tofauti na mashabiki wa Simba,” anasimulia.

Maisha yake ya Sweden

Mwaka 2007, Machupa alimaliza mkataba Simba na kutimkia Denmark ambako alicheza mwaka 2008 na mwaka uliofuatia alikwenda nchini Sweden ambako ndiko amestaafia soka.

“Nilipostaafu sikutaka kurudi nyumbani, nilihamishia makazi yangu huku ambako nimeoa na nina mtoto mmoja,” anasimulia.

Anasema mkewe ni raia wa Tanzania, ambaye walitoka naye nchini na kuhamia Sweden.

Anasema alipenda maisha ya Sweden kwa kuwa ni nchi ambayo haina mambo mengi na kila raia kule ana haki.

“Sweden ni nchi fulani poa sana, unapata haki zako ipasavyo na kila raia anayeishi huku ana haki sawa, ni nchi fulani ambayo sijui hata niielezee vipi,” anasema Machupa ambaye anaishi kwenye mji wa Stockholm.

Anasema nchini humo kuna mastaa wengi wa Tanzania na mara kadhaa wamekuwa wakitembeleana akiwamo bondia, Awadh Tamim ambaye wanaishi mji mmoja.

“Kama nilivyosema Sweden ni nchi fulani hivi, haina mambo mengi, ukiishi kwenye hii nchi lazima ufurahie maisha, tupo Watanzania wengi huku, na mara moja moja huwa tunapata nafasi ya kutembeleana au kukutana,” anasema.

Anasema makazi yake amehamishia nchini humo, lakini amewekeza nchini na anafanya biashara ya ufugaji wa kuku na sungura jijini Dar es Salaam, biashara inayomuingizia kipato.

“Maisha sasa ni magumu mno, bila kujiongeza huwezi kufanikiwa, hata vijana huko nyumbani niwashauri tu wajifunze kuweka akiba, hakuna pesa ambayo haiwekwi akiba, unapopata mshahara usitumie wote ukijua mwezi ujao utapata tena, weka akiba,” alisisitiza.

Hakuitendea haki Simba hapa

Machupa anakumbuka namna alivyocheza Simba kwa mafanikio ikiwamo kutwaa ubingwa wa ligi bila kufungwa, sanjari na kuifunga Zamalek kwenye mashindano ya kimataifa.

“Tulipoifunga Zamalek tulikuwa vizuri mno, tulitoka kuzifunga timu nyingine kubwa tu Afrika kabla ya Zamalek,” anasema na kuongeza.

“Nakumbuka tuliwahi kutwaa ubingwa wa ligi bila kufungwa, lakini ndoto yetu wakati ule haikutimia, tulikuwa na malengo ya kuwa bingwa wa Afrika.

“Malengo ambayo hatakutimia na binafsi naona sikuitendea haki Simba kwenye hilo, kama ningepata nafasi ya kurudia enzi, hili ni jambo ambalo ningetamani litokee, lakini ndiyo hivyo kwa upande wangu haiwezekani, labda kwa wadogo zangu wa kizazi cha sasa au kijacho,” anasema.

Tofauti anayoiona Simba sasa

Machupa ambaye aliichezea Simba kwa miaka tisa mfululizo anasema, Simba ya wakati wao sio hii ya sasa.

“Vitu vingi vimebadilika, mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo sasa ni tofauti, Simba ya sasa ina uwanja wake wa mazoezi, wakati ule sisi tulikuwa tunahangaika wapi tukafanye mazoezi.

“Mishahara ya wachezaji kuna wakati ilikuwa shida, lakini sasa mambo hayo ni kama yametulia, ila kinachonisikitisha tu kwa timu yangu hiyo na hata Yanga ni kutowapa nafasi washambuliaji wazawa.

“Nakumbuka wakati sisi tunacheza pale mbele tulisimama mimi, Madaraka Seleman, Yusuf Macho, Emanuel Gabriel wote ni wazawa, hata Yanga washambuliaji wazawa tulipata nafasi, lakini Simba ya leo wanaocheza ni Meddie Kagere, Clatous Chama, Deo Kanda, ukienda Yanga ni yale yale.

“Wazawa wanakosa nafasi ya kuimarika, mfano Simba mzawa ambaye anacheza mara kwa mara utakuta ni John Bocco naye kuna wakati anaanzia bechi.

Anasema ufike wakati timu hizo mbili zianze kuwapa nafasi washambuliaji wazawa kwani wapo wengi wazuri kushinda hata baadhi ya hao wageni inaowasajili na kuwalipa pesa nyingi.

“Wakiwapa nafasi wazawa, hakuna shaka tutatengeneza washambuliaji wazuri wa Taifa Stars, lakini pia mpango wa kupunguza wachezaji wa kigeni, binafsi sioni kama una afya kwenye soka letu.

“Wasajiliwe hata 20 kwa kila klabu, lakini wawe ba uwezo ambao vijana wa Kitanzania hawana, ili tujifunze kupitia kwao, lakini sio mchezaji wa kigeni anakuja, uwezo wake hata alionao mchezaji wa Ndanda mzawa ni afadhali, hii sio sawa,” anasema.

Amtaja Juma Kaseja

Kiwango cha kipa wa KMC na Taifa Stars, Juma Kaseja kimeelezewa na Machupa kuwa ni matunda ya kujitunza.

Machupa amemtaja Kaseja kama kipa waliyepata naye mafanikio Simba mwanzoni mwa mwaka 2000 ikiwamo kuifunga Zamalek na kutwaa ubingwa bila kufungwa, ingawa Machupa amestaafu, Kaseja bado ni kipa tegemeo kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars) mpaka sasa.

“Kaseja ni zaidi ya mchezaji, anajua nini abachokifanya na uwezo wake ni matunda ya kujitunza, anaishi kwa kufuata misingi ya kiprofesheno, ambayo wachezaji wengi wa Kibongo hawaifuati.

“Unajua ukiwa mchezaji wa kulipwa hata kama unalipwa laki tatu wewe ni profesheno, inabidi uiheshimu mno hatua uliyofikia, lakini Watanzania wengi hawafuati miiko hiyo,” anasema.

Anasema Kaseja ukiachana na mazoezi, lakini anajua kujitunza kisoka, muda wa kupumzika arapumzika, muda wa mazoezi atafanya mazoezi, wengine wajifunze kupitia yeye,” alisema Machupa ambaye anajiandaa kuwa mshauri wa soka nchini.

Advertisement