BOCCO ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA

STRAIKA aliyeifunga Simba mara nyingi kwenye rekodi za mashindano yote, John Bocco ‘Adebayor’ 

Muktasari:

Hakuna mchezaji yeyote wa ndani na nje anayeifikia rekodi ya Bocco kuinyanyasa Simba akiwa na Azam ambayo ilitaka kumpa mkataba wa kishikaji.

STRAIKA aliyeifunga Simba mara nyingi kwenye rekodi za mashindano yote, John Bocco ‘Adebayor’ amesaini miaka miwili Msimbazi.

Hakuna mchezaji yeyote wa ndani na nje anayeifikia rekodi ya Bocco kuinyanyasa Simba akiwa na Azam ambayo ilitaka kumpa mkataba wa kishikaji.

Nahodha huyo aliyeipandisha daraja Azam, amesaini mkataba wa miaka miwili kuhitimisha mazungumzo yaliyoanza wiki iliyopita ambapo juzi Jumanne yalikamilika huku Bocco akiridhia dau la Sh48 milioni na mshahara wa Sh4 milioni ambao atapewa na Simba.

Simba imemaliza ishu hiyo wakati ambapo Bocco alishafanya mazungumzo ya awali na Yanga ambao bado akili zao zinaonekana kujikita zaidi kwenye furaha ya ubingwa na mkwara wa Mwenyekiti wao, Yusuf Manji ambaye amebwaga manyanga. Lakini Mwanaspoti linajua kwamba Manji hataondoka Yanga licha ya wadau na vikundi mbalimbali kujipanga kwenda kumwomba abadili uamuzi.

Chanzo hicho kinasema kuwa Simba wameanza kufanya usajili wao kimya kimya ambapo sasa watahamia kwa kipa wa Azam, Aishi Manula na beki wa Mbao FC, Mrundi Yusuph Ndikumana ambaoa wote mikataba yao imemalizika. Aishi anatakiwa pia na Singida United.

“Bocco tayari amesaini mkataba huo akiwa mchezaji huru, ni mchezaji mzuri ambaye atawapa changamoto akina Laudit Mavugo, pia Aishi naye mazungumzo yanaendelea na muda wowote yanaweza kukamilika, tunamuhitaji Aishi ili ampe changamoto Daniel Agyei,” kilisema chanzo hicho.

“Tulikuwa tunamuhitaji zaidi Mbaraka Yusuph lakini anaonekana kutokuwa tayari kurudi Simba, ni kama ilivyo kwa Shomary Kapombe naye hana utayari huo japo tunahitaji huduma zao.

“Usajili tutakaoufanya utazingatia mahitaji yetu kwa msimu ujao.”

Mbaraka yeye ana ofa tatu mkononi ambazo ni Yanga ambao wapo tayari kumpa Sh50 milioni kwa miaka miwili, Azam FC wenyewe wamedaiwa kutoa ofa ya Sh 15 milioni kwa mkataba wa mwaka mmoja na Singida United ambao ofa yao haijawekwa wazi.

Kiongozi huyo alisema kuwa wachezaji ambao wanadengua kusaini mikataba mipya huenda wasiwabembeleze tena ni pamoja na Ibrahim Ajibu anayetajwa kuwaniwa na Yanga, Jonas Mkude na Abdu Banda.

Habari za ndani pia zinasema wakongwe Mwinyi Kazimoto na Method Mwanjali ambao mikataba yao inamalizika nao hawatapewa mikataba mipya wakati kipa Manyika Peter Jr atapelekwa Lipuli kwa mkopo.