BMT: Michezo mingine ruksa kurudi viwanjani wiki hii

Muktasari:

Rais John Pombe Magufuli aliruhusu michezo kurejea Juni Mosi baada ya kusitishwa tangu Machi 17 ili kupunguza mikusanyiko na kuchukua tahadhari ya janga la corona linalotikisa dunia.


Dar es Salaam.Wakati likijiandaa kukutana na vyama vya michezo tofauti na soka wiki hii  Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limesema chama ambacho hakikuwasilisha programu yao kwao hawatoruhusiwa kuendelea na michezo huku vingine vikiruhusiwa kurejea viwanjani wiki hii.

BMT hivi karibuni ilivitaka vyama vya michezo kuwasilisha programu zao za namna zitakavyoendesha mashindano yao huku vikichukua tahadhari wakati huu wa janga la virusi vya corona, ikiwa ni siku kadhaa tangu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuruhusu  soka kuendelea huku michezo mingine ikiandaliwa utaratibu wa kurejea.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha ameiambia MCL Digital kuwa kabla ya Ijumaa ya wiki hii michezo mingine pia itapewa muongozo wa namna ya kurejea uwanjani.

Amesema michezo hiyo ni ile ambayo imewasilisha programu zao BMT tu na ile ambayo haikufanya hivyo haitaruhusiwa kuendelea na programu yoyote wakati huu.

"Ambao hawakuwasilisha programu zao kwetu maana yake hawana kitu cha kufanya, hivyo hawatoruhusiwa kuendelea na chochote wakati huu," alisema Neema.

Alisema baadhi ya vyama ndivyo vimewasilisha programu zao wakiwamo netiboli, wavu na kikapu.

"Siwezi kuvikumbuka vyote, lakini sio vingi ambavyo vimeleta kwetu hizo programu, ingawa hivi vyama vikubwa vikubwa vingi vimewasilisha na ndivyo vitaruhusiwa kuendelea na matukio yao ya kimichezo," amesema.

Amesema jana ndiyo wamemaliza kupitia programu hizo na kabla ya Ijumaa watakutana na vyama hivyo kwa ajili ya kupeana muongozo na kuendelea na programu zao za kimichezo za mwaka huu kama kawaida.

"Kikubwa ni tahadhari, hata hivyo kwa sasa wanaruhusiwa kuendelea na mazoezi yao na mapema iwezekanavyo wiki hii tutakutana nao ili kupeana miongozo waendelee na programu zao kama kawaida," amesema.