BATA BATANI : Ole anogesha mzuka Man United

Tuesday January 8 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND.OLE Gunnar Solskjaer anajaribu kuteka akili ya kila mchezaji kwenye kikosi cha Manchester United ili wapambane kwa ajili yake. Kocha huyo wa muda, amekichukua kikosi chake na kwenda nacho huko Dubai kutafuta hali ya joto, huku wakijiandaa na mechi yao ngumu kabisa dhidi ya Tottenham Hotspur Jumapili ijayo.

Kwenye mtoko huo wa Dubai, Solskjaer amewaambia wachezaji wake kwamba habanwi mtu, kila mtu afanye anavyojisikia na kuwasisitiza kwamba jukumu la kuitafutia mambo mazuri Man United ni la kila mtu. Jambo hilo limedaiwa kuwafanya wachezaji wa Man United kuona kwamba sasa wanaheshimika na kusimamiwa kama watu wazima.

Kwenye ziara hiyo amekosekana mchezaji, Paul Pogba, lakini ataungana na wenzake baada ya siku mbili baada ya yeye kubaki England kufanyiwa matibabu kutokana na maumivu aliyopata kwa kuchezewa rafu na Jonjo Shelvey kwenye mechi dhidi ya Newcastle United. Man United imefikia kwenye hoteli ya One&Only Royal Mirage Arabian Court.

Solskjaer amekuwa akisifika kwa kubadili upepo kwenye klabu ya Man United tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu baada ya Jose Mourinho kufutwa kazi.

Wachezaji wameambiwa hivi, ratiba ya chai asubuhi ni saa 3, lakini sio lazima, mchezaji anaweza kwenda kupata kifungua kichwa muda wowote anaotaka mwenyewe. Solskjaer amewaambia wachezaji wake hakuna kufanya mambo ya kulazimishana, akifanya hivyo kuangalia akili zao kama watajiweka sana na kujiendeesha kama watu wazima.

Mastaa hao wa Man United wameambiwa kwamba kutakuwa na mazoezi magumu siku moja kwa siku na mlo wa mchana itakuwa lazima kwa wachezaji kula pamoja na ule mlo wa usiku, ambapo chakula kitakuwa tayari kuanzia saa 2 usiku.

Baada ya hapo, Solskjaer amewaamini wachezaji wake na kuwaambia watafahamu wenyewe muda wa kwenda kulala na si kulazimishana kama watoto. Kocha huyo raia wa Norway ameipeleka timu yake kwenye ziara hiyo ili kuwafanya wachezaji wao wacheze kwa ajili yake na kupata matokeo.

Hadi sasa Solskjaer ameisimamia Man United kwenye mechi tano na kushinda zote, huku ikiwa kwenye timu hiyo kwa siku 20 tu. Wachezaji wengi wameonekana kurudi kwenye ubora wao, akiwamo Romelu Lukaku, ambaye alisema: “Yeah, nadhani sio mimi tu bali ni kila mchezaji. Nadhani kwa sasa tumekuwa sisi wenyewe na hakika ni jambo zuri kwa kila mchezaji kufurahia kucheza na kushinda mechi ni kitu muhimu. Sisi ni Manchester United na tutajaribu kuingia uwanjani na kushinda kila mechi.”

Kocha Mourinho aliweka utaratibu mgumu kwenye timu hiyo na kuwafanya wachezaji kutokuwa na amani katika kuitumikia timu. Lakini, Solskjaer amebadili kila kitu na kuwaongoza wachezaji hao kama watu wazima bila ya kuwawekea masharti ya kijinga. Wachezaji wameruhusiwa kushikirikiana kijamii, licha ya kwamba safari yao hiyo ya Dubai imelenga zaidi katika kufanya mazoezi ya ndani ya uwanja ili kujiweka fiti kabla ya kwenda kumalizia msimu. Solskjaer amewapa uhuru wachezaji wake ili kutambua akili zao kama wanaweza kujiongoza wenyewe kama wachezaji profesheno.

Advertisement