Azam yazitaka tatu za Biashara

Muktasari:

Katika mchezo huo Cioaba anatakiwa apate pointi tatu ili kuweza kuweka utulivu kwa mabosi wake ambao wanashauku ya kutaka kupata matokeo.

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba leo Ijumaa atakuwa na kibarua kingine kigumu katika mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Chamazi saa moja jioni, akihitajiwa kuzoa alama zote tatu dhidi ya wapinzani wao walioanza kutakata.
Katika mchezo huo Cioaba anatakiwa apate pointi tatu ili kuweza kuweka utulivu kwa mabosi wake ambao wanashauku ya kutaka kupata matokeo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Msemaji wa klabu hiyo, Jaffer Idd alisema maandalizi ya mchezo yamefanyika vizuri na wapo tayari kufanya vizuri katika mchezo huo.
Jaffer alisema katika mchezo huo beki wao,Abdallah Kheri 'Sebo' anarejea uwanjani baada ya kukosekana kwa muda mrefu.
"Sebo amerejea kwahiyo katika kucheza kwake italingana na mwalimu kwenye mahitaji yake, lakini yupo fiti tayari," alisema.
Cioaba anatakiwa kupata ushindi baada ya katika michezo yake ya awali kupata kufungwa mmoja na kutoka sare mmoja.
Cioaba alipoteza 1-0 Ruvu Shooting na kutoka sare 0-0 dhidi ya Kagera Sugar, tangu amrithi Etienne Ndayiragije aliyeteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars baada ya kufungashiwa virago.