Azam yapania makubwa kwa Triangle United

Muktasari:

Azam inatarajiwa kuwakaribisha Triangle United katika mchezo huo wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika utaofanyika Jumapili 15 majira ya saa 10 jioni Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Kombe la FA, Azam FC wamesema hawatawaangusha mashabiki wao watakaposhuka uwanjani kuivaa Triangle United ya Zimbabwe katika mchezo wa raundi ya kwanza Kombe la shirikisho Afrika utaofanyika Jumapili 15 majira ya saa 10 jioni Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Kocha msaidizi wa Azam, Idd Cheche alisema Azam inafahamu umuhimu wa mashindano hayo kwa nchi hivyo ni lazima kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kusonga mbele.

“Kupitia mashindano haya nchi yetu imefanikiwa kupata fedha kutokana na idadi ya timu 4 zilizoingia mwaka huu, ambazo ni Azam, Simba, Yanga na KMC bahati mbaya wenzetu Simba na KMC wamewahi kutolewa sasa ni jukumu letu kufanya vizuri kuliwakilish taifa kwa ujumla.” 

“Azam tumejipanga vizuri na tunaahidi kutowaangusha mashabiki zetu na taifa zima kwa ujumla tumejipanga vizuri na tumeufahamu udhaifu wetu na kuufanyia kazi hivyo tutahitaji kupata matokeo kwetu kisha tukapate matokeo ugenini,” alisema Cheche.

Akizungumzia michezo yao ya kirafiki waliyocheza hivi karibuni.

“Tumecheza na Transit Camp, Friends Rangers na Pan African’s zote tumeshinda. Mechi hizi zimetujenga zaidi tumetambua makosa yetu na kuyafanyia kazi hivyo tunatarajia kupata ushindi nyumbani na ugenini,” alisema.

Kocha Cheche aliwazungumzia wapinzani wao Triangle United kuwa si timu ya kubezwa.

“Mpinzani wetu sio dhaifu, mpaka timu imepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo sio ya kubezwa hawa Triangle United ni wazuri ila wana madhaifu yao na mpira wa miguu ni mchezo wa kutumia madhaifu ya mpinzani wako hivyo tutajitahidi kutumia madhaifu ya Triangle kupata matokeo” alisema.

Cheche alisema habari njema kwa Azam ni kurejea kikosini kwa majeruhi Mudathir Yahya ameanza mazoezi na wenzake.

“Mudathir amerejea na ameanza mazoezi na wenzake ila nahodha Aggrey Morris na Abdallah Heri bado hawajajiunga na wenzao” alisema.

 “Mashabiki waondoe shaka juu ya timu yetu wajitokeze kwa wingi wajaze uwanja tunaahidi hatutawaangusha ushindi wa Azam ni ushindi wa Tanzania kwa ujumla hivyo watu wajitokeze kwa wingi kutupa hamasa,”  alisema Cheche.