Azam yanasa kifaa kingine

Saturday August 1 2020

 

Siku mbili baada ya kumsajili kiungo Awesu Awesu kutoka Kagera Sugar, Azam FC imeendelea kutikisa dirisha la usajili baada ya kutangaza kukamilisha usajili wa kiungo Ally Niyonzima kutoka Rwanda mwenye umri wa miaka 24.

Kiungo huyo anayechezea timu ya Taifa ya Rwanda 'Amavubi' amejiunga na Azam FC akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Rayon Sports ya Rwanda kumalizika mwaka huu.

Zoezi la usajili wa Niyonzima anayemudu vyema kucheza nafasi ya kiungo wa kati na kiungo mshambuliaji lilikamilika rasmi leo Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Azam, Mzizima likishuhudiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' baada ya mchezaji huyo kukamilisha vipimo vya afya.

Akizungumza muda mfupi baada ya kutambulishwa rasmi, kiungo huyo ambaye alikuwa pia kwenye rada za Yanga, alitoa shukrani kwa wote waliofanikisha usajili wake.

“Nawashukuru wote waliowezesha mimi kusajiliwa hapa. Mimi kinachonileta hapa ni kufanya kazi hivyo inabidi akili yangu niweke katika kazi. Nimezungumza na Emmanuel Mvuyekure kuhusu Azam, ameniambia mambo mengi mazuri kuhusu Azam.

Malengo yangu ya kwanza ni kutumika. Mimi siku zote ni mpambanaji na nimekuwa naweka mawazo na kichwa changu kwa timu ambayo imenisajili. Mashabiki wa Azam wategemee mazuri na makubwa lakini yote ni Mungu ndiye anatoa nafasi ili uweze kufikia kwenye malengo yako,” alisema Niyonzima.

Advertisement

Advertisement