Azam yamrejesha kundini Amoah, Chirwa ngoma bado

Muktasari:

 

  • Beki Daniel Amoah amerejea katika kikosi cha Azam baada ya kukaa nje ya Uwanja kwa miezi Saba alipokuwa kiuguza majeraha ya kifundo Cha mguu.

Dar es Salaam. Azam Fc imemrejesha beki wake wa kulia Daniel Amoah katika usajili wa dirisha dogo baada ya mchezaji huyo kupona majeraha ya kifundo cha mguu.

Amoah raia wa Ghana aliumia msimu uliopita na kupelekwa Afrika Kusini kufanyika upasuaji hivyo kutakiwa kukaa nje ya uwanja kwa miezi tisa.

Azam haikumjumuisha mchezaji huyo katika usajili wao msimu huu kutokana na kuona atakaa nje muda mrefu.

Afisa Habari wa Azam, Jaffar Iddi alisema wameamua kumsajili tena Amoah katika dirisha dogo kutokana na kuridhishwa na maendeleo yake kiafya.

"Baada ya kufanyiwa upasuaji tuliambiwa angekaa nje ya uwanja kwa miezi tisa hivyo hatukumsajili katika usajili wetu wa msimu huu kwa sababu tuliona asingetumika msimu mzima"

"Hata hivyo sasa hivi Amoah amerejea uwanjani baada ya kupona majeraha yake kwa haraka kabla ya miezi tisa aliyotakiwa kukaa nje ya Uwanja haijatimia na ndio maana tumeamua kumrejesha tena kwa kumsajili kwenye dirisha dogo"alisema Jaffar.

Akizungumzia usajili wa Obrey Chirwa, Iddi alisema wanasubiri uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka Misri.

"Shirikisho Soka Tanzania (TFF) limeshaomba ITC ya Chirwa huko Misri na inatakiwa itumwe ndani ya siku 14 ambazo zinaisha leo hivyo tunasubiri hadi kesho ili tuone imekuaje.

"Chirwa tulimsajili baada ya kuja na barua ya kuruhusiwa na klabu yake aliyokuwa akiichezea huko Misri na Kama asingekuja na hiyo barua ambayo ilisainiwa na Rais wa hiyo klabu aliyokuwa akiichezea tusingemsajili.

"Sasa hizo habari kwamba ana matatizo na klabu yake tunazisikia tu na hatujui nini kilitokea huko nyuma baada ya yeye kuondoka kuja huku," alisema Iddi.