Azam yampa ulaji beki Mghana

Muktasari:

Amoah raia wa Ghana, aliumia msimu uliopita na kupelekwa Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji na alitakiwa kukaa nje ya uwanja miezi tisa. Dirisha la usajili lilifunguliwa Novemba 15 na litafungwa Desemba 15.

Dar es Salaam. Azam FC imemrejesha beki Daniel Amoah katika usajili wa dirisha dogo, baada ya kupona jeraha la kifundo cha mguu.

Amoah raia wa Ghana, aliumia msimu uliopita na kupelekwa Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji na alitakiwa kukaa nje ya uwanja miezi tisa. Dirisha la usajili lilifunguliwa Novemba 15 na litafungwa Desemba 15.

Ofisa Habari wa Azam Jafari Idd alisema wamemsajili Amoah baada ya kuridhishwa na maendeleo ya afya.

“Amoah amerejea uwanjani baada ya kupona majeraha kwa haraka kabla ya miezi tisa aliyotakiwa kukaa nje ya uwanja haijatimia, ndiyo maana tumeamua kumrejesha tena kumsajili katika dirisha dogo,”alisema Idd.

Akizungumzia usajili wa Obrey Chirwa, Idd alisema wanasubiri uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka Misri.

“Shirikisho Soka Tanzania (TFF) limeshaomba ITC ya Chirwa huko Misri na inatakiwa itumwe ndani ya siku 14 ambazo zinaisha leo, hivyo tunasubiri hadi kesho ili tuone kama itakuwa imefika au vinginevyo.

“Chirwa tulimsajili baada ya kuja na barua ya kuruhusiwa na klabu yake aliyokuwa akicheza Misri na kama asingekuja na hiyo barua ambayo ilisainiwa na rais wa klabu hiyo tusingemsajili”, alisema Ofisa Habari huyo.

Mchezaji huyo raia wa Zambia, anakwenda kuungana nyota mwenzake wa zamani wa Yanga, Mzimbabwe Donald Ngoma.