Azam yakubali yaishe kwa dili la Sure Boy Yanga

UONGOZI wa klabu ya Azam umemuweka sokoni kiungo wao Salum Abubakari 'Sure Boy' baada ya mchezaji huyo kuomba kuondoka katika klabu hiyo.

Kupitia kwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thabit Zakaria amesema uongozi wa klabu hiyo umekubaliana na mchezaji husika baada ya kuomba kuondoka.

"Sure Boy licha ya kuhusishwa na klabu mbalimbali huyu ni mchezaji wetu sisi, lakini yeye mwenyewe amekutana na viongozi na amewaomba kutafuta changamoto mpya baada ya kukaa hapa kwa muda mrefu,"

"Awali tulikuwa watulivu baada ya yeye mwenyewe kusema hana ofa yoyote lakini pia hana mpango wa kuondoka ndio maana tukawaambia Yanga kwamba mchezaji huyu hauzwi,"

Zaka alifunguka zaidi na kusema baada ya mchezaji huyo kukaa na viongozi wake wameamua kumuweka mchezaji huyo sokoni.

"Yupo sokoni sasa hivi mchezaji wetu na timu yoyote ambayo itamuhitaji basi wawasiliane na sisi,"

Kuondoka kwa Sure Boy unakuwa muendelezo wa nyota wa kikosi hiko kuondoka baada ya awali kutoka Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula na John Bocco.