Azam yaichapa Simba yabeba tena Kombe la Mapinduzi

Muktasari:

  • Azam imetwaa ubingwa bila kupoteza hata mchezo mmoja katika mashindano ya kuadhimisha Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar, likiwa ni la tano kwao, kwani ailishatwaa mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019 katika msimu huu wa 13 tangu michuano hii ilipoasisiwa mwaka 2007.

PEMBA.MABAO ya Mudathir Yahya na Obrey Chirwa yalitosha kuizamisha Simba kwa mara nyingine tena katika mechi ya fainali, baada ya jana Jumapili kuisaidia Azam kupata ushindi wa mabao 2-1 na kunyakua taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019.

Hii ni mara ya tatu Simba kufungwa kwenye mechi ya fainali baada ya mwaka juzi kuchapwa bao 1-0 na Azam katika michuano ya Mapinduzi 2017 na mwaka jana ililala tena kwa mabao 2-1 katika fainali ya Kombe la Kagame 2018 iliyofanyika jijini Dar.

Simba ikiundwa na wachezaji wengi wa kikosi cha pili na wale wa vijana, wakitoka kupata kushangilia ushindi wa mabao 3-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria juzi Jumamosi ilijikuta ikishindwa kufurukuta mbele ya vijana wa Hans Pluijm.

Mudathir Yahya alianza kuishtua Simba kwa kufunga bao la kuongoza kwa shuti kali dakika ya 44, bao lililokuja kusawazishwa na beki, Yusuf Mlipili kwa kichwa katika dakika ya 63 akimalizia kona ya Shiza Kichuya.

Hata hivyo Chirwa aliyeibuka Mfungaji Bora wa michuano hiyo alifunga bao lake la tano kwa kichwa katika dakika ya 72 akimalizia krosi tamu ya beki, Nicholas Wadada.

Licha ya Simba iliyokuwa ikiongozwa na Haruna Niyonzima aliyeupiga mpira mwingi kuonyesha soka zuri kwa kuchuana na nyota wa Azam, lakini ilionyesha wapinzani wao walidhamiria kutetea taji lao kwa mara ya tatu na kubeba jumla.

Azam imebeba taji hilo bila kupoteza hata mchezo mmoja katika michuano hiyo ya kuadhimisha Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar likiwa pia ni la tano kwao, kwani ilishatwaa mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019 ikiwa msimu huu wa 13 tangu michuano hii ilipoasisiwa mwaka 2007 ambapo Yanga ikiwa ya kwanza kulibeba.

Kwa matokeo hayo, Azam imenyakua zawadi ya Kombe, Medali za Dhahabu na Sh 15 Milioni, huku Simba iliyonyakua taji hilo mara tatu tangu ianzishwe wakipewa medali za fedha na Sh 10 Milioni za ushindi wa pili.

Timu hizo zinzreje Dar es Salaam kuajili ya maandalizi na mapambano ya Ligi Kuu Bara, huku timu zote mbili zikiwa zinakimbizana kusaka ubingwa.