Azam yahamia Prisons yabeba kiungo

Muktasari:

Kiungo Ismail Aziz anakuwa wa tatu kusajiliwa na Azam FC ukiwa ni muendelezo wa kusuka kikosi chao tayari kwa msimu ujao.

Azam FC wameendelea na kazi ya kukisuka kikosi chao baada ya kumnasa kiungo wa Prisons FC, Ismail Aziz ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili.

Aziz ambaye amekuwa katika kiwango bora msimu uliomalizika amefuzu vipimo vya afya alivyofanyiwa leo Jumatatu Agosti 3, 2020 tayari kwa kuingia mkataba na Azam waliomaliza Ligi katika nafasi ya tatu.

Azam ilimsafirisha kiungo huyo juzi tayari kwa mchakato wa usajili huo baada ya kumvutia kocha Aristica Cioaba.

Usajili huo wa Aziz utamfanya kuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Azam ndani ya dirisha hili la usajili lililofunguliwa Agosti Mosi mwaka huu.

Mapema Azam imeshakamilisha usajili wa Kiungo Awesu Awesu (Kagera Sugar), Mnyarwanda Ally Niyonzima (Rayon Sport), Ayoub Lyanga (Coastal Union.

Mapema Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdukarim Amin 'Popat' amesema baada ya kuwafanyia mchujo wachezaji mbalimbali waliowavutia msimu huu sasa wanafanya kazi ya kukamilisha usajili wa wale ambao wamekubaliana kuja kukiboresha kikosi chao.