Azam waitaka rekodi ya AFC Leopard

Muktasari:

Leopards walichukua kombe hilo kuanzia 1982-1984, huku Azam wakichukua 2016-2018 na kesho wamepanga kupambana kutetea ubingwa huo.

MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, Azam FC kesho Jumapili atakuwa na kibarua kigumu cha kutetea ubingwa wao dhidi ya KCCA ya Uganda.
Azam  wamekuwa mabingwa wa michuano hiyo ambapo kama watashinda mechi hiyo ya fainali watavunja rekodi iliyowekwa na timu ya AFC Leopards ya Kenya ambao waliwahi kuchukuwa kombe hilo mara tatu mfululizo.
Leopards walichukua kombe hilo kuanzia 1982-1984, huku Azam wakichukua 2016-2018 na kesho wamepanga kupambana kutetea ubingwa huo.
Azam walitinga fainali baada ya kuifunga Maniema kwa mikwaju ya penalti 5-4, huku KCCA waliifunga Green Eagles 4-3 michezo ya nusu fainali.
KCCA na Azam FC walikutana katika mchezo wa hatua ya makundi ambapo Azam walikubali kichapo cha bao 1-0.
Azam wametamba kushinda mchezo huo ili kuweka rekodi ya michuano hiyo tangu waanze kushiriki.
Mchezaji wa Azam FC, Idd Kipagwile alisema wanatambua kwamba KCCA ni timu nzuri na ina nyota wazoefu lakini watahakikisha wanapambana kulinda kombe hilo.
“Unajua hawa jamaa walitufunga mchezo wa nyuma sasa hilo jambo hatutaki litokee mara mbili, wana timu nzuri lakini hii ni fainali lazima tupambane,” anasema.