Azam tatizo lipo hapa tu

AZAM imepoteza pointi tano katika Ligi Kuu baada ya juzi usiku kulazimishwa sare na JKT Tanzania, huku wakitoka kupoteza bao 1-0 kwa Mtibwa Sugar, ikielezwa kukosekana kwa Obrey Chirwa kumekwamisha Prince Dube kuendeleza moto wake wa kutupia mabao nyavuni.

Katika mechi hizo mbili alizokosekana Chirwa katika safu ya ushambuliaji, kumeipa wakati mgumu Azam kufumania nyavu na kupata ushindi kulinganisha na mechi za nyuma alipokuwepo.

Chirwa alianza kukosekana katika mchezo wa ugenini dhidi ya Mtibwa waliowachapa bao 1-0 na pia hakuwepo juzi walipotoka sare ya bao 1-1 nyumbani na JKT Tanzania.

Licha ya kuhusika kwa mabao 10 ya Azam katika mechi saba za mwanzo walizoshinda huku akicheza sambamba na Chirwa, Dube ameshindwa kufurukuta kwa kushindwa kufunga bao na hata kupiga pasi ya mwisho.

Kabla ya kupoteza mbele ya Mtibwa na kutoka sare dhidi ya JKT Tanzania, wawili hao walionekana kuwa moto wa kuotea mbali ambapo katika jumla ya mechi saba walizocheza dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union, Prisons, Mbeya City, Kagera Sugar, Mwadui FC na Ihefu SC, washambuliaji hao wawili kwa pamoja walifunga jumla ya mabao 10 kati ya 14 ambayo Azam ilikuwa imepachika.

Chirwa amekosekana kutokana na kusumbuliwa na majeraha na benchi la ufundi la Azam chini ya Kocha Aristica Cioaba katika mechi za hivi karibuni limekuwa likimtumia ama Never Tigere au Richard Djodi.

Hata hivyo, kocha msaidizi wa Azam, Bahati Vivier alisema hakuna uhusiano baina ya kukosekana kwa Chirwa na kupoteza pointi tano katika mechi zao mbili.

“Huu ni mpira na kuna wakati unaweza kufanya vizuri na muda mwingine ni bahati tu inayokosekana,” alisema kocha huyo.