Azam ni kimya kimya

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuletea mambo ambayo yamechangia Azam FC ambayo ilianzishwa Juni 24, 2007 kuwa miongoni mwa timu imara ambazo zinaweza kutwaa ubingwa msimu huu, ikishindania kinyang’anyiro hicho na klabu kongwe za Simba na Yanga.

MATAJIRI wa Ligi Kuu Bara, Azam FC wanaendelea kusalia kileleni mwa msimamo baada ya kucheza mechi 13 wakifikisha pointi 33 wakiwa hawajapoteza mechi hata moja huku wakifunga mabao 17 na wao wakifungwa matatu.

Mwanzo wa simu timu zilizokuwa zinatazamiwa kuchukua ubingwa kwa msimu wa 2018/19 ni Simba na Yanga, huku Azam FC ikiachwa mbali na kinyang’anyiro hicho, lakini kwa sasa upepo umebadilika na Azam FC ndio inayoongoza.

Azam FC ni kama inamkimbiza mwizi kimya kimya kwani licha ya kuwa mbele kwa michezo dhidi ya Simba na Yanga, lakini imekuwa na matokeo mazuri mfululizo na kuanza kuonesha dalili njema kama timu ambayo inaweza kutwaa ubingwa msimu huu.

Mwaka 2008 Azam FC, ilipanda Ligi Kuu Bara na mpaka sasa inakuwa ni miaka 10, lakini imefanikiwa kuchukua ubingwa mara moja (2014/15) na msimu huu imeonesha nia ya kurudia rekodi hiyo.

Mwanaspoti linakuletea mambo ambayo yamechangia Azam FC ambayo ilianzishwa Juni 24, 2007 kuwa miongoni mwa timu imara ambazo zinaweza kutwaa ubingwa msimu huu, ikishindania kinyang’anyiro hicho na klabu kongwe za Simba na Yanga.

BENCHI LA UFUNDI

Azam mwanzoni mwa msimu imeanza kwa kuboresha benchi lake la ufundi kwa kuwaajili makocha wawili ambao wana rekodi nzuri katika soka la Tanzania ili kuimarisha kikosi chake ambacho ni wazi kina kiu ya mafanikio msimu huu.

Makocha hao ni Mdachi Hans Van Pluijm ambaye ilimchukua kutoka Singida United na alikuwa hapo kwa muda wa mwaka mmoja na baada ya kutoka Yanga ambako alifanya kazi kama mkurugenzi wa ufundi.

Baada ya kumpata Pluijm, kazi ya ilimnasa, Juma Mwambusi ili kuwa msaidizi akifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Iddi Cheche ambaye yupo katika nafasi hiyo kwa muda mrefu na kuifanya Azam kuwa imara katika benchi la ufundi na kuwa na makocha watatu waliokamalika.

Benchi la ufundi la Azam pia lina, Alando Philip ambaye ni meneja lakini amecheza soka na Idd Abubakar ambaye ni kocha wa makipa ambaye pia ana uwezo mkubwa. Azam ni wazi benchi lake la ufundi ni imara kuliko timu nyingi za Ligi Kuu na ni wazi kuna dalili njema msimu huu imekuwa fit zaidi na inaweza kutwaa ubingwa kutokana na kujiandaa vizuri.

USAJILI

Baada ya kurekebisha benchi lake, Azam ilifanya usajili wa wachezaji wa maana ambao wengi wanafanya vizuri mpaka sasa kulingana na kila nafasi ambazo wanacheza nyota hao. Wachezaji waliosajiliwa na Azam ni beki wa kulia, Nicholas Wadada ambaye amekuwa katika kikosi cha kwanza na ameitendea haki nafasi hiyo tofauti na msimu uliopita kulikuwa na mapungufu na muda mwingine alikuwa akicheza, Himid Mao ambaye ni kiungo mkabaji. Wengine ni mshambuliaji, Donald Ngoma ambaye licha ya kusajiliwa akiwa majeruhi na kukosa baadhi ya mechi, tayari amefunga mabao matatu mpaka sasa, Tafadwa Kutinyu naye amefunga matatu.

Danny Lyanga naye amepachika mabao mawili, huku Mudathir Yahya akionyesha kiwango bora katika safu ya kiungo mkabaji na Hassan Mwasapili licha ya kucheza mechi chache lakini amefanya vizuri pia.

Ditram Nchimbi ndiye mchezaji pekee ambaye amesajiliwa na Azam na ameshindwa kupata nafasi ya kucheza, lakini wote wamefanya vizuri na kuifanya timu hiyo kuwa imara kwa usajili ilioufanya tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Katika kujiimalisha zaidi Azam kwenye dirisha dogo la usajili ilimnasa, Obrey Chirwa ambaye ni mmoja kati ya mastraika wazuri kwani misimu miwili iliyocheza Yanga alifunga mabao 12 kila msimu na alikuwa mfungajo Bora wa Kombe la FA.

WAZOEFU

Azam mbali ya kufanya usajili wa wachezaji wa maana lakini imefanikiwa kubaki na wachezaji wake wazoefu ambao wameijenga timu hiyo kuzidi kuwa imara zaidi ya msimu uliopita.

Nahodha Aggrey Morris, Yakub Mohammed, Abdallah Kheri ‘Sebo’, Bruce Kangwa, Frank Domayo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wamekuwa muhimili imara wa Azam msimu wakicheza sambamba na maingizo mapya na kuifanya timu hiyo kuimarika.

Ukuta wa wachezaji wazoefu wa Azam unalindwa na mabeki Morris, Mohammed, Sebo, Kangwa, Mwasapili na Wadada ambao wanacheza kwa nyakati tofauti wamefungwa mabao matatu katika mechi 13.

Uzoefu wa wachezaji waliokuwa katika kikosi cha Azam umechangia kuwa na kikosi imara ambacho huenda mwisho wa msimu ikawa timu ambayo inawania ubingwa.

UWANJA WA NYUMBANI

Kwa misimu miwili, Azam imefungwa mara mbili tu katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Kagera Sugar msimu wa 2016-17 na dhidi ya Yanga msimu uliopita.

Azam imeonekana kuimarika na kuutumia vizuri uwanja wake huo wa Azam Complex na hata msimu huu haijapoteza mechi yoyote katika uwanja huo.

Hata katika viwanja vingine ambapo imecheza mechi zake 13 na kuzidi kukusanya pointi tatu na kupata sare tatu pekee hadi sasa. Ni wazi Azam ina matumizi mazuri ya uwanja wake wa nyumbani na huenda ukawa silaha kubwa ya kuvuna pointi nyingi hapo ingawa mechi zake za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga zitachezwa katika Uwanja wa Taifa.

Uamuzi wa Azam kucheza mechi zake za nyumbani dhidi ya watani hao wa jadi ni kutokana na sababu za kimaslahi zaidi. Ifahamike Azam haina mashabiki wengi na uwanja wake ni mdogo kulinganisha na ule wa Taifa ambao unaweza kuwakusanya wengi wa Simba na Yanga.