Azam kuipasua Simba

Wednesday May 15 2019

 

By Thomas Ng'itu

KIPAUMBELE cha mabosi wa Simba kwa sasa ni kuona kwanza, wanatetea ubingwa wao kisha chini kwa chini wakisuka mikakati ya mazungumzo ya kuwapa mikataba mipya baadhi ya mastaa wake.

Mwishoni mwa msimu huu, kuna mastaa takribani sita kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ambao, mikataba yao inafikia ukingoni na hilo limeanza kuzifanya timu zingine hasa Yanga na Azam FC, kuanza kupita chini kwa chini kushawishi nyota hao wabadili gia angani.

Hata hivyo, taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti limepenyezewa ni kwamba, mabosi wa Azam FC wamekiri kuchemka kuwaachia wachezaji wake muhimu kutua Simba msimu uliopita na sasa wanataka kurekebisha makosa.

Taarifa ni kuwa mabosi hao wa Azam wameanza mikakati ya kuipasua Simba kwa kuhakikisha inawarudisha nyumbani nyota wanne, Aishi Manula, Erasto Nyoni, John Bocco na Shomary Kapombe ambao waliitema Azam na kutua Simba.

Mastaa hawa wote waliachana na Azam FC mwishoni mwa msimu uliopita, baada ya Wana Lambalamba hao kubadilisha sera ya uendeshaji klabu hiyo ambapo, ilitangaza kupunguza matumizi na gharama zingine za uendeshaji na kugoma kulipa ada wakati wa kusaini dili jipya.

Kwa sasa wachezaji wote hao ndio wameibeba Simba msimu uliopita kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na sasa wote wako kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Advertisement

Sasa mabosi wa Azam wamekiangalia kikosi chao na mateso wanayoyapata na kufikia uamuzi kwamba, wanakwenda kuwarudisha kikosi mastaa wake hao ili kuifanya kuwa moto kama misimu mitatu iliyopita.

Kwa sasa Bocco ameifungia Simba mabao 14 huku Nyoni akitengeneza safu ya ukuta wa zege na Manula analinda lango kwa umakini mkubwa.

Kwa upande wa Kapombe, ambaye pia alikuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, alifanya vizuri ingawa alikabiliwa na majeraha tangu atue Simba huku muda mwingi akiwa nje ya uwanja.

Azam iliachana na wachezaji hao baada ya kuamua kubana matumizi, lakini msimu huu wameanza kutumia tena fedha katika kukisuka upya kikosi chake na wana kiu kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Msimu huu haina chake kwenye ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini inaweza kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa kupitia mlango wa uani kama itaichapa Lipuli FC kwenye fainali ya Kombe la FA.

Pia, katika kuhakikisha wamejipanga kikamilifu, Azam FC imewaongeza mikataba mipya mastaa wake muhimu akiwemo Yakub Mohamed, Bruce Kangwa na Abdallah Kheri ambao walianza kuzengewe na Simba na Yanga.

“Kuna hiyo mipango ila tunasubiri muda ufike kwanza, tunahitaji kuwarudisha kikosi wachezaji wetu ambao waliifanya Azam kuwa tishio. Tunajipanga kwa wote ila tukishindwa basi hata wawili tu akiwemo Kapombe,” alisema mtoa habari wetu ndani ya kikosi hicho.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa bosi mmoja wa Azam tayari ameanza kufanya mazungumzo ya chini chini na baadhi ya wachezaji hao ingawa Simba nao wameshtukia mchezo huo.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin (Popat) hakuweza kupatikana hata kupitia simu yake ya kiganjani.

Lakini, Mratibu wa Azam FC, Philip Alando alikiri kuwa amekuwa akizisikia taarifa hizo zikizungumzwa sana lakini, bado halijajadiliwa rasmi kwenye vikao vya klabu hiyo.

“Nasikia sana suala hilo na hata jana (juzi) baada ya mechi na Simba, nilisikia jambo hilo, lakini haya mambo bado hayapo kwani hatujaanza kuzungumzia masuala ya usajili mpya,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa taarifa hizo zinaweza kuzungumzwa sana kutokana na wachezaji hao wote mikataba yao inafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.

Mabosi wa Azam wamekuwa makini sana wanapotekeleza mambo yao hasa ya usajili kama ilivyokuwa kwa kocha wao wa zamani Hans Pluijm, ambaye alihusishwa kutua Chamazi lakini, mabosi hao waligoma katakata na baadaye akatua.

KAKOLANYA NDANI

Wakati hilo la kuwarudisha mastaa hao likishika kasi, kuna taarifa pia Azam wako katika harakati za kumnasa kipa Beno Kakolanya. Kwa sasa Kakolanya ni mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na Yanga ingawa pia, Simba wanamfuatilia wakitaka kwenda kumpa changamoto Manula.

Azam wanahitaji kipa huku ikielezwa kuwa Razak Abarola, huenda akatemwa mwishino mwa msimu ujao.

Meneja wa Kakolanya, Haroub Seleman alisema: “Beno aliniambia kuna mtu kutoka Azam amempigia simu kuhusu hayo mambo ya usajili, lakini hawajaja rasmi mezani kama ilivyo kwa Simba, hakuna timu ambayo tumekaa nayo na kufikia makubaliano.

“Kikubwa tunachohitaji ni nafasi ya kucheza pamoja na maslahi mazuri kwa mchezaji, ingawa kila timu ina faida yake,” alisema Haroub.

Meneja wa Azam, Philipo Alando alisema: “Tuna makipa wawili Razak Abalora, ambaye mkataba wake unamalizika 2020 na Mwidin Ally. Hata hivyo, huwezi kuanza kuzungumzia usajili wa wachezaji wakati hajapatikana kocha mpya. Hili ni jukumu la kocha.”

Advertisement