Azam iliwapoteza Yanga hapa tu

Muktasari:

Yanga imepoteza mchezo wa pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara ikiwa chini ya kocha mpya, Luc Eymael.

SIO mwanzo mzuri katika kikosi cha Yanga baada ya kocha mpya, Mbelgiji Luc Eymeal kupoteza mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar na jana Jumamosi dhidi ya Azam Fc. Pia, atakuwa na kibarua kingine Jumatano mbele ya Singida United ugenini.
Katika mchezo wa jana Jumamosi dhidi ya Azam, Yanga ilifanya mambo kadhaa ambayo yalisababisha kushindwa kupata ushindi wakati huo huo wapinzani wao wakitumia maeneo hayo kama njia ya zao kupata ushindi jambo ambalo walifanikiwa baada ya dakika tisini kumalizika.
Mwanaspoti ambalo lilikuwa karibu likifuatilia mchezo huo liligundua mambo hayo ambayo Yanga waliyafanya mpaka kufungwa wakati wapinzani wao Azam FC, waliyatumia na kuweza kupata pointi tatu.
MASTRAIKA BADO
Katika kikosi cha Yanga kwenye mechi na Azam kilianza na mshambuliaji mmoja David Molinga, ambaye alionekana kuwa bora hasa kipindi cha kwanza akisumbua ngome ya ulinzi ya Azam iliyokuwa chini ya mabeki wa kati Daniel Amoah pamoja na kinda Oscar Masai.
Molinga aliwasambua mabeki hao lakini hakuwa na msaada kwa mshambuliaji wa pili ambaye alikuwa akicheza Mapinduzi Balama, Haruna Niyonzima pamoja na Kabamba Tshishimbi kulingana na shambulizi ambavyo lilikuwa.
Baada ya kuonekana katika eneo hilo kuna shida na mabeki wa Azam kuwa bora, Eymael aliwaingiza washambuliaji wawili kwa wakati tofauti Ditram Nchimbi na Yikpe Gnamein ambao, walikwenda kutimiza idadi ya mastraika watatu asilia ambao kwa pamoja walishindwa kuwa bora mbele ya safu ya ulinzi ya Azam.

WAPYA
Kikosi cha Yanga katika mechi na Azam kilianza na wachezaji wapya saba ambao wote wapya walisajiliwa katika dirisha kubwa ambao ni kipa Farouk Shikalo, Lamine Moro, Ally Mtoni, Haruna Niyonzima, Mapinduzi Balama, Molinga na Patrick Sibomana.
Katika kipindi cha pili waliwaingiza wachezaji wapya wawili Nchimbi na Yikpe jambo ambalo lilitimiza wachezaji tisa waliocheza kwenye mechi hiyo wote wapya jambo ambalo kiufundi si rahisi kwenda kupata matokeo mazuri dhidi ya Azam ambao timu yao ipo pamoja kwa muda mrefu.
YANGA BILA MPIRA
Wachezaji wa Yanga walionekana kuwa bora pale timu yao inapokuwa na mpira, lakini wanapopoteza walikuwa na makosa mengi. Kwanza, kuna baadhi ya wachezaji ambao mara chache walikuwa wakijihusisha na shughuli ya kukaba kama Niyonzima na Molinga.
Jambo hili na kutokuwa makini na kufanya makosa wanapokuwa hawana mpira, Azam waliyatumia kupenya na kuingia kwa urahisi katika eneo la Yanga ila walikosa umakini wa kutengeneza nafasi za kufunga. Kama Yanga wangecheza na timu ambayo ina wezo wa kupiga presha wanapokuwa hawana mpira huenda wangepoteza kwa idadi kubwa ya mabao.
Azam walionekana kumiliki mpira muda mwingi katika maeneo mengi kwani, wachezaji wa Yanga walishindwa kuwa makini katika kukaba.
EYMAEL BADO ANAKAZI
Eymael bado anakazi kubwa ya kuifanya Yanga kuwa na kikosi bora hasa kucheza kwa kuelewana kwani, maeneo mengi wameonekana kuwa na shida kama safu ya ushambuliaji, kiungo na hata ulinzi ambapo hufanya makosa mengi mara kwa mara.
Anatakiwa kutenga muda wa kutosha katika mazoezi ya Yanga na kufanyia kazi mapungufu kama timu inapokuwa haina mpira ni kitu gani  wachezaji wafanye kulingana na wapinzani walivyo. Pia, wanapokuwa na mpira wanatakiwa kushambulia kwa aina gani.
NIYONZIMA, TSHISHIMBI
Kabla ya Yanga kumsajili Niyonzima katika dirisha dogo walionekana kutokuwa na kiungo mshambuliaji mbunifu aina yake jambo ambalo hata kufika kwake katika mechi tatu za ligi ambazo amecheza mpaka bado hajaoneasha hilo.
Niyonzima, ambaye amebeba matumaini makubwa ya wapenzi wa Yanga katika eneo kiungo, ameonesha umahiri wa kumiliki mpira na kupiga pasi nyingi ambazo hazina faida kwa maana zinakwenda pembeni, lakini wakati huo huo unaweza kukuta timu inashambulia kwa haraka akipewa mpira anageuka nyuma.
Hivyo vyote ndio alifanya katika mechi ya Azam ambayo viungo wa timu pinzani Salum Abobukar 'Sure Boy' na Brayson Raphael kutawala eneo hilo muda wote kwani, walipokuwa na mpira wanapanga kwenda mbele zaidi badala ya kwenda nyuma.
AZAM MBINU
Katika mchezo huo Azam walionekana kuingia na mbinu ya kutaka kumiliki mpira kwa muda mrefu, kushambulia kwa taratibu huku wakipiga pasi fupi fupi ambazo ziliwafanya kufika langoni mwa Yanga mara chache lakini, kwa mashambulizi hatari.
Mbinu hiyo ya Azam iliwanufaisha baada ya kupata bao la kuongoza dakika 26 ambalo beki Ali Mtoni Sonso alijifunga.
CIOABA KUWAIGA KAGERA
Mwanaspoti liliona kama kocha wa Azam, Aristica Cioaba wala hakuwa na kazi kubwa kwani ni wazi alionekana kuifatilia mechi ya Yanga wakipoteza nyumbani kwa mabao 3-0, dhidi ya Kagera Sugar.
Cioaba alichukua mbinu za Kagera Sugar kumiliki mpira kwa muda mwingi, kupiga pasi fupi fupi, kucheza kwa nidhamu, kuwaheshimu wapinzani na kuzuia njia za Yanga kushambulizi ambazo ni kutumia mawinga na mabeki wa pembeni.
CHIRWA, NGOMA BADO
Azam dhidi ya Yanga walianza na washambuliaji wawili Obrey Chirwa na Shabani Chilunda ambao, walionekana kukosa umakini na kushindwa kutimiza majukumu yao ya kufunga.
Chirwa, Chilunga na Donald Ngoma ambaye aliingia baadaye walionekana kupata shida mbele ya Moro na Sonso.
MWAISABULA HUYU HAPA
Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema Azam waliingia katika mchezo huo wakiifuatilia vya kutosha Yanga pindi wanapokuwa hawana mpira na pale wanapokuwa na mpira.
"Yanga licha kufanya usajili lakini timu haichezi kwa kuelewana mbele ya Azam ambao, wameimatrika na kucheza vizuri. Yanga wanafanya makosa ya mara kwa mara jambo ambalo wangecheza na timu makini basi habari ingekuwa nyingine," alisema Mwaisabula na kuongezea kuwa kocha wa Yanga Eymael bado ana kazi ya kufanya kikosini kwake.