Azam hiyoo, inazidi kupaa tu
Azam FC imeendeleza moto wake kwenye Ligi Kuu Bara baada ya leo Jumanne kuichapa Ihefu mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.
Timu hiyo sasa imefikisha pointi 21 na kuzizidi timu kongwe Simba na Yanga pointi nane ingawa watani hao wa jadi wana mechi mbili mkononi
Ikicheza kwa kiwango bora Azam ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 55 kupitia kwa Ayoub Lyanga na aliyefunga kwa shuti kali akimalizia krosi ya Prince Dube.
Azam iliendelea kuliandama lango la Ihefu na kufanikiwa kupata bao la pii lililofungwa na Iddi Selemani'Nado' kwa kichwa akimalizia pasi safi ya Dube.
Kipigo hicho ni kama kimemkaribisha vibaya kocha mpya wa Ihefu ,Zubery Katwila ambaye muda mwingi wa mchezo alionekana amesimama akiwaelekeza wachezaji wake.
Katwila alijiunga na Ihefu Juzi Jumapili akitokea Mtibwa Sugar alikodumu tangu 1999 akiwa mchezaji na baadae kupewa kazi ya ukocha.
Ihefu imeonekana kujitahidi kucheza vizuri lakini ugeni wa ligi na uzoefu mdogo wa wachezaji wa kikosi hicho ndio umekuwa ukiwaponza na kupoteza michezo yao mingi.
Mapaka sasa Ihefu imecheza michezo saba, imeshinda mmoja na kupoteza sita na iko nafasi ya pili kutoka mwisho kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tatu.