Azam FC yaweka rekodi ya miaka 10

Wednesday October 21 2020
azam pic

Dar es Salaam. Azam FC haikamatiki kwenye Ligi Kuu Bara, baada ya jana kuichapa Ihefu SC kwa mabao 2-0 na kuzidi kuwatimuliwa vumbi wapinzani wake wakubwa, Simba na Yanga, ikiendelea kukaa kileleni mwa msimamo sambamba na kuandikisha rekodi mpya.

Timu hiyo imefikisha pointi 21 baada ya kushinda michezo saba iliyocheza mpaka sasa msimu huu ikiwa ni mara ya kwanza tangu ianze kucheza Ligi Kuu Bara mara ya kwanza mwaka 2010.

Azam ilianza ligi msimu huu kwa kuifunga Polisi Tanzania bao 1-0, kisha ikaichapa Coastal Union mabao 2-0, ikaifunga Mbeya City bao 1-0, ikaibamiza Prisons bao 1-0, ikainyuka Kagera Sugar mabao 4-2 na kuiadhibu Mwadui mabao 3-1 kabla ya jana kuifunga Ihefu mabao 2-0.

Tangu mwaka 2010, Azam ilipoanza kucheza Ligi Kuu haijawahi kupata ushindi mfululizo katika mechi saba za mwanzo wa ligi, hivyo msimu huu kuwa mara ya kwanza kuweka rekodi hiyo.

Katika mchezo wa jana mabao ya Ayoub Lyanga na Iddi Selemani ‘Nado’ yalitosha ‘kumkaribisha’ kocha mpya wa Ihefu, Zubery Katwila ambaye alianza kukinoa kikosi hicho siku moja kabla ya mechi.

Lyanga alifunga bao la kwanza dakika ya 55 kwa shuti kali akimalizia krosi ya Prince Dube kabla ya Nado kufunga la pili katika dakika ya 84 kwa kichwa akiunganisha pasi ya Dube. Mabao hayo mawili yameifanya Azam kufikisha 14 kwenye ligi sawa na Simba, hivyo kuwa timu pekee zilizoonyesha kuwa na safu kali za ushambuliaji zilizofunga mabao mengi mpaka sasa.

Advertisement

Kocha msaidizi wa Azam, Vivier Bahati alisema ni furaha kwao kuweka rekodi hiyo, na anaamini wataendelea kucheza kwa kiwango bora katika mechi zote zijazo kwani wamedhamiria kutwaa ubingwa msimu huu.

“Tunachotaka sisi ni kucheza vizuri na kushinda kila mchezo.Unapoweka rekodi inabidi kuendelea kupambana zaidi ili kuvunja rekodi hiyo na kuweka mpya,” alisema Vivier.

“Tumedhamiria msimu huu kuhakikisha kuwa tunatwaa ubingwa na ndio maana kila mechi kwetu tunaichukulia umuhimu na kuhakikisha tunapata pointi tatu.”

REKODI MIAKA 10

Azam ilianza msimu wa 2010/2011 kwa kucheza mechi saba na kupata ushindi katika mechi tatu, ikipoteza tatu na kutoa sare mchezo mmoja ilhali msimu wa 2011/2012 katika mechi saba za mwanzo ilishinda nne, ikatoka sare michezo miwili na kupoteza mmoja.

Katika msimu wa 2012/2013 timu hiyo ilipata ushindi wa michezo mitano na sare mbili katika mechi saba ilizocheza mwanzoni mwa ligi wakati ule wa 2013/2014 ilishinda mechi mbili na kutoka sare mechi tano, huku msimu wa 2014/2015 ilishinda michezo minne, ilipoteza miwili na sare moja.

Katika msimu wa 2015/2016, Azam ilicheza michezo saba mwanzoni mwa ligi na kushinda sita huku ikitoka sare mchezo mmoja, wakati msimu wa 2016/2017 ilishinda michezo mitatu, ilitoka sare michezo miwili na kupoteza miwili huku msimu wa 2017/18 katika mechi saba ilishinda tatu na kutoka sare michezo minne.

Msimu wa 2018/2019, timu hiyo ilipata ushindi katika michezo mitatu na kutoka sare michezo minne katika mechi saba ilizocheza wakati msimu uliopita timu hiyo ilianza ligi na katika michezo saba ya mwanzo ilishinda minne, ilipoteza miwili na kutoka sare mchezo mmoja.

Katika mchezo mwingine uliofanyika jana saa 8:00 mchana kati ya Ruvu Shooting ilitoka sare ya bao 1-1 na KMC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

KMC ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Andrew Vincent ‘Dante’ katika dakika ya 26 kabla ya Ruvu Shooting kusawazisha kupitia kwa Shaban Msala kwenye dakika ya 56.

 

Advertisement