Azam FC yautaka ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la FA

Muktasari:

  • Azam FC wanatarajia kushuka uwanjani kesho kuumana na Ruvu Shooting wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa mwisho katika ligi dhidi ya Mtibwa Sugar kwa kukubali kipigo cha mabao 2-0

Dar es Salaam. Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi amesema sasa nguvu zao wanazihamishia katika mataji mawili ya Ligi Kuu na Kombe la FA kwa lengo lao ni kuhakikisha wanayatwaa yote.

Mwambusi ameyasema hayo Dar es Salaam leo, baada ya kutua wakitokea visiwani Zanzibar ambako wametwaa taji la Mapinduzi kwa kuifunga Simba bao 2-1.

Alisema bado wananafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi na FA na wapo tayari kwa mapambano huku akiweka wazi kuwa hawahofii timu yoyote wapo kwaajili ya kushindana na sio kushindwa.

Azam kwa sasa ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 baada ya kucheza mechi 17, huku Yanga ikiongoza na pointi 50 baada ya mechi 18, huku Simba ikiwa ya tatu na pointi zake 33 na mechi 14.

"Kwasasa tunaangalia makombe mawili yaliyobaki na sisi tukiwa kama washindani tunashiriki Ligi kuu na FA tunaimani kubwa ya kuonyesha ushindani na kutwaa ubingwa kabisa," alisema Mwambusi.

Mwambusi alisema sasa wanajiandaa na Ruvu Shooting wanatambua ni wazuri hivyo wamejipanga kuhakikisha wanashinda kila mchezo ulio mbele yao.