Azam FC yapigwa tena, Himid afichua tatizo

Muktasari:

Azam FC inahitaji wachezaji wanaoweza kujisukuma wenyewe kwa asilimia kubwa ili waweze kuleta matokeo mazuri na yenye muendelezo wa kushika nafasi za juu na kupata hata nafasi za kushiriki michuano ya kimataifa kwa sababu watapata kuonekana na timu za nje wanaposhiriki mashindano hayo.

MAMBO sio mazuri kwa Mhalonzi Hans Pluijm katika mbio zake za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuchapwa tena jana Alhamisi na Tanzania Prisons uwanjani Sokoine bao 1-0.

Azam iliingia uwanjani ikitaka kurekebisha makosa yake baada ya kutoka kupata sare dhidi ya Lipuli, lakini mambo yakazidiwa kuwa mabaya.

Kabla ya kulazimishwa sare na Lipuli, Azam ilikuwa imetoka kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar huku ikilazimishwa sare pia na Alliance FC kwenye uwanja wake wa nyumbani pale Chamazi.

Bao pekee kwenye mchezo huo lilipachikwa wavuni na Jumanne Fadhili kwa mkwaju wa penalti baada ya straika wa Azam, Yakubu Mohemend kunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Kwa ushindi huo, Prison inayonolewa na kocha Mohamed Adolf Rishard, imendelea kuweka rekodi ya kutopoteza michezo yake kwenye uwanja wa nyumbani. Kwa sasa imefikisha pointi 29 kwenye msimamo ikishinda mechi tano.

Hata hivyo Himid Mao anaifuatilia timu yake hiyo ya zamani na amefichua kinachoikwamisha isisonge mbele kulingana na uwekezaji iliyofanya.

Himid alisema mawasiliano mabovu baina ya wachezaji ni tatizo mojawapo linaloifanya Azam isitishe kama matarajio ya wingi.

Matajiri hao wanashika nafasi ya pili kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya mechi 23 na kukusanya alama 49.

Himid alisema nyota wote waliopata nafasi ya kucheza Azam wanatakiwa kuwa wamoja na kufahamu kuwa wanachezaji timu isiyo na shida wala kundi kubwa la mashabiki hivyo hawana presha kulinganisha na klabu za Simba na Yanga.

“Azam ni timu yenye ubora kutokana na kuweza kumiliki kila mahitaji ya mchezaji ili aweze kuwa katika uimara unaotakiwa, hivyo wachezaji wanatakiwa wajitume na kuwa wamoja ili kuisaidia timu ifikie malengo ya haraka japo naomba niweke wazi kuwa bado haijashindwa sana kulingana na mfumo wa soka la Tanzania,” alisema.

“Wachezaji wanaonunuliwa Azam wanatakiwa kujituma na kupambania timu sio timu kwa sababu haina kundi kubwa la mashabiki kama zilivyo Simba na Yanga ambazo wanapewa presha,” alisema.

Pia aliongeza ili timu hiyo iweze kufanikiwa inahitaji wachezaji wanaoweza kujisukuma wenyewe kwa asilimia kubwa ili waweze kuleta matokeo mazuri na yenye muendelezo wa kushika nafasi za juu na kupata hata nafasi za kushiriki michuano ya kimataifa kwa sababu wachezaji watapata kuonekana na timu za nje wanaposhiriki mashindano ya kimataifa na michezo ya kirafiki na timu za nje.