Azam FC yaivaa Simba akili kwa Waethiopia

Wednesday August 14 2019

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Kikosi cha Azam FC kimeingia kambini leo Jumatano kwa maandalizi ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, wameahidi kuitumia mechi hiyo kujiimarisha kwa mechi ya Fasil Kenema ya Ethiopia.

Azam FC imeweka kambi katika hosteli yao  iliyopo Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam tayari kwa mchezo huo utakaopigwa wikiendi hii Uwanja wa Taifa, ikiwa ni ufunguzi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020.

Msemaji wa Azam FC, Jafar Idd Maganga amesema, kikosi hicho kipo chini ya makocha wao wote,  Mrundi Ettiene Ndayiragije ambaye alikuwa na majukumu na Taifa Stars kwenye mechi ya kuwania kufuzu fainali za CHAN ameungana na Idd Cheche.

''Timu inaendelea na maaandalizi kama kawaida na inafanya mazoezi mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni ili kupata kikosi chenye ubora zaidi. Tunacheza na Simba ambao ni mabingwa wa ligi na sisi Kombe la FA hivyo utakuwa mchezo mzuri,"alisema Jafar Idd.

"Pia, kama nilivyosema, mechi hiyo itakuwa sehemu ya sehemu ya maandalizi ya mechi yetu ya marudiano na Fasil Kenema.''

Katika mchezo wa kwanza ambao Azam FC walikuwa ugenini nchini Ethiopia, walifungwa bao 1-0 ambapo Jafar Idd amesema, pamoja na kupoteza kwao imekuwa nzuri kwa sababu wamepata nafasi ya kuanzia ugenini jambo linalowapa nafasi nzuri.

Advertisement

"Safari hii ratiba ya mechi zetu za CAF imekuwa nzuri kwa sababu ni tofauti na miaka mingine ambayo tulikuwa tunanzia nyumbani na kumalizia ugenini jambo lilikuwa linatupa wakati mgumu katika mashindano kama hayo ya kimataifa."

 

 

Advertisement