Azam FC wazidi kukomaa

LICHA ya kupoteza mchezo wao wa kwanza, kocha msaidizi wa Azam FC, Bahati Vivier amesema kupoteza kwao hakujawatoa katika mbio za kupigania ubingwa msimu huu.

Azam ilifungwa juzi jioni bao 1-0 na Mtibwa Sugar ukiwa ni mchezo wa kwanza kupoteza msimu huu baada ya kucheza mechi nane na kupoteza mchezo moja.

Bahati alisema: “Kuna mechi nyingi bado mbele, hivyo kupoteza katika mchezo huu sio kwamba ndio tumetoka katika mbio, tunaamini tutaendeleza kupata pointi tatu katika mechi zijazo.”

Akizungumzia kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake nyota Salum Abubakar na Obrey Chirwa, alisema: “Sisi tuna wachezaji wengi sana, kwa hiyo sio kukosekana kwao ndio tatizo, hawa nao ni wachezaji wetu na wanastahili kucheza na wamecheza vizuri, tunajipanga kwa ajili ya mechi zijazo.”

Wakati huohuo Kaimu Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Vicent Barnabas alisema licha ya kupata ushindi bado hajajipa nafasi ya kuwa kocha mkuu.

“Siwezi kusema kwamba mimi ni kocha mkuu, hapa mwenzangu aliyetoka alikaa takribani misimu sita kama kocha msaidizi, Meck na yeye alikaa muda mrefu kama kocha msaidizi kwa hiyo sio suala la kulizungumzia kipindi hiki,” alisema Barbanas.

Azam FC licha ya kupoteza mchezo huo bado inaendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 21 katika mechi nane ilizocheza, huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Yanga yenye pointi 19 katika mechi saba ilizocheza, ilhali biashara United ni ya tatu ikiwa na pointi 16.