Azam FC wataja ishu nne

KOCHA msaidizi wa Azam FC, Mrundi Vivier Bahati amesema ugumu na ushindani mkali uliopo Ligi Kuu Bara, unatokana na mambo manne, yatakayowafanya wachezaji waongeze bidii na umakini katika kazi zao.

Alitaja mambo hayo manne ni mwaka jana kushuka timu nne moja kwa moja ambazo ni Ndanda, Singinda, Lipuli, Alliance, huku Mbao ikiondolewa katika hatua ya mtoani ‘play off’ na Ihefu ya mkoani Mbeya.

Bahati aliendelea kutaja sababu nyingine ni timu zimefanya usajili mzuri, makocha wanafanya kazi yao kwa umahiri na kujiwekea mazingira mazuri ya kuepuka kushuka daraja.

“Sababu nne nilizotaja ndizo zinafanya ligi iwe na ushindani wa hali ya juu, kwa upande mwingine inasaidia wachezaji kufanya kazi zao kwa umakini ili kutimiza malengo ya timu zao na wenyewe kukuza thamani zao,” alisema nakuongeza.

“Tumeshinda mechi tano, sio kwamba ilikuwa ni kazi rahisi, tulipambana na wapinzani wetu ambao nao walihitaji kuzivuna hizo pointi tatu kwetu, lakini kwa wakati huo bahati haikuwa upande wao, bado kazi inaendelea tunajipanga zaidi ili tufikie malengo yetu ya msimu huu,”alisema.

DUBE, CHIRWA KUFANYA MAAJABU

Ukiachana na alivyozungumzia ugumu wa ligi, alisema straika wao Prince Dube anajituma kuhakikisha anazitikisa nyavu za wapinzani wao na mpaka sasa ndiye anaongoza kwa kuwa na mabao matano kwenye msimamo wa wafungaji.

Alisema kwa bidii zake anaona timu yao itazalisha mabao mengi akisaidiana na Obrey Chirwa, anaoamini wana nguvu yakulazimisha mashambulizi mbele ya mabeki wagumu.

“Sina kwamba wachezaji wengine ni wabaya, nazungumzia Dube na Chirwa jinsi ambavyo hata ukuta wa wapinzani ukibana wanajua kupenyenza mpaka kufunga,” alisema.