Azam FC hii gusa unate aseee!

Muktasari:

Mwanaspoti limeangalia namna timu hiyo imefanya maaandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao.

KLABU ya Azam ni wazi imeanza vibaya katika Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa 1-0 na FC Kenema.

Lakini hilo haliwazuii wao kushindwa kupindua matokeo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi kati ya Agosti 23 mpaka 25.

Kabla ya mchezo huo Azam walikuwa wameshafanya maandalizi kwa ajili ya msimu mpya kwa kuhakikisha wanafanya usajili mzuri ili kuweza kutoa ushindani katika mashindano ambayo wanashiriki.

Mwanaspoti limeangalia namna timu hiyo imefanya maaandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao.

USAJILI WAO

Azam inayonolewa na Kocha Ettiene Ndayiragije, imefanya usajili wa hesabu nzuri kwa kuangalia maeneo ambayo ambayo yanashida na kujazia.

Ettiene alihakikisha anasajili mshambuliaji, na alifanikiwa kumpata Dally Ella Djodi na Seleman Ndikumana ambao wana uzoefu wa kutosha ilikwenda kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji.

Pia alihakikisha eneo la kiungo linakuwa zuri na alimchukua Emmanuel Mveyakure, Idd Seleman, Albakassim Suleiman ambao wameonekana kuwa na tija katika kikosi chao.

Ni usajili mzuri Ettiene ameufanya kwani ameangalia maeneo muhimu na kuyajazia nyama ili timu ifanye vizuri.

Pia amewaongezea mkataba wachezaji Daniel Amoah, Salmin Hoza, Obrey Chirwa, Bryson Raphael na Benedict Haule.

JEZI ZA NYUMBANI NA UGENINI

Kila klabu inapokuwa inaingia katika msimu mpya huwa wanabadili muundo wa jezi, hio sio Bongo tu, hata huko kwa wenzetu walioendelea.

Kwa upande wa Azam licha ya kubadili jezi mara kwa mara, wamejitahidi kuweka msimamo katika kuendeleza rangi za jezi zao.

Azam wanatumia jezi nyeupe wanapokuwa wapo ugenini na za bluu wanapokuwa nyumbani.

UWANJA WA NYUMBANI

Matajiri hawa wa Ligi Kuu Bara wanamiliki uwanja wao binafsi kule Chamazi uliokamilika kila kitu kinachotakiwa kwa timu inayoshiriki Ligi Kuu.

Imezipiga bao Simba na Yanga kwenye upande wa uwekezaji, lakini wamekuwa kimya kutozungumza chochote kile na kuacha kazi yao ya uwanjani ndio iongee.

Simba hivi sasa ikiwa chini ya mwekezaji wao tajiri, Mohammed Dewji ndio wameonekana kuamka zaidi na kuweka mkazo katika uwanja wao uliopo Bunju kuhakikisha unatengenezwa kisasa.

BAJETI YAO KIDUCHU

Licha ya Azam wanatajwa ndio matajiri Ligi Kuu Bara, lakini CEO wa timu hiyo Abdulkarim Amin ‘Popat’ mara kwa mara amekuwa akisema wao sio matajiri kwani hilo limekuwa likiwapa tabu wakati wa usajili.

Popat aliwahi kukaririwa na Mwanaspoti akisema “Sisi hatuwezi kutoa pesa nyingi kama ambavyo Simba wanatoa katika usajili, sisi tunatoa pesa ya kawaida.”

Lakini Mwanaspoti linafahamu Azam walishuka na kuweka kiwango cha Sh15 milion kwa usajili wa wachezaji wa ndani, hali ambayo imewafanya wapishane na nyota wengi pindi wanapowaitaji.

UFUNDI WA MAKOCHA

Kocha Ettiene Ndayiragije anasifika kwa ufundi wa kucheza soka la chini la haraka, hilo limejionesha akiwa katika kikosi cha Mbao, KMC na sasa Azam.

Ettiene pia ni muumini wa soka la vijana, alilithihirisha hilo tangu akiwa katika kikosi cha Mbao, KMC mpaka hivi sasa na hawajawahi kumwangusha na kutokana pia na falsafa zake.

Soka lake la mbinu limekuwa changamoto kwa timu nyingi anazokutana nazo, hilo ameweza kulionyesha hata katika timu ya Tanzania, ambayo alikuwa kaimu kocha mkuu baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Emmanuel Amunike kutimuliwa.